Site icon A24TV News

Wananchi wa kijiji cha Igombola kata ya Lupembe Wilaya ya Njombe wamelalamikia ubovu wa miundombinu ya barabara .

Na Emmanuel octavian

Katika mkutano wa hadhara wa mkuu wa Wilaya ya Njombe baadhi ya wakazi hao akiwemo Peter Kyamani na Lucy Mligo Wamesema ubovu wa barabara hasa wakati wa masika umekuwa ukikatisha mawasiliano pamoja na mazao kuozea shambani.

Awali diwani wa kata ya Lupembe Michael Mbanga amesema changamoto ya miundombinu ya barabara ni kubwa hususani katika kipindi cha masika kwani shughuli za kiuchumi zimekuwa zikisimama.

Mtaalam wa ujenzi toka Wakala wa barabara za mijini na vijjini TARURA wilaya ya Njombe Mhandisi Mussa Mwansule amekiri kuwapo kwa changamoto ya miundombinu hiyo huku akisema itatazamwa katika bajeti ya mwaka ujao kwani kwa sasa hakuna bajeti.

Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Njombe Kissa Kasongwa amesema ni muhimu TARURA wakaona namna ya kwenda kufanya marekebisho hata kwenye maeneo korofi badala ya kuacha kabisa barabara kusubiri mwaka wa fedha ujao huku akiwataka watumishi kuwasikiliza madiwani wanapowafuata kuwaeleza kero mbalimbali.

Mkuu wa wilaya ya Njombe katika ziara yake ametembelea na kufanya mikutano katika kijiji cha Igombola kata ya Lupembe pamoja na vijiji vya Madeke na Mfiriga kata ya Mfiriga