Site icon A24TV News

PROFESA KIKULA AAINISHA MIKAKATI YA TUME YA MADINI KWENYE UBORESHAJI WA SEKTA YA MADINI

Na Mwandishi wa A24Tv

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa Serikali kupitia Tume ya Madini imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha Sekta ya Madini inanufaisha kila mwananchi na kuinua sekta nyingine za kiuchumi na uchumi kuendelea kukua kwa kasi.

Profesa Kikula ameyasema hayo leo Oktoba 13, 2022 jijini Mwanza kwenye kikao cha nne cha Baraza la Wafanyakazi kilichoshirikisha Kamishna wa Tume ya Madini, Janet Lekashingo, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, Katibu wa TUGHE Mkoa wa Dodoma Nsubisi Mwasandende, Mwakilishi wa Kamishna wa Kazi – Ofisi ya Waziri Mkuu, Goodluck Luginga, watendaji kutoka Tume ya Madini Makao Makuu na kutoka Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa chenye lengo la kujadili na kutatua changamoto katika utendaji kazi wa Tume ya Madini.

Amesema kuwa mikakati iliyowekwa ni pamoja na ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini kupewa kipaumbele ambapo kwa sasa wananchi wameanza kutoa huduma kwenye migodi ya madini iliyoanzishwa nchini na kujipatia kipato, uboreshaji wa miundombinu na huduma nyingine za jamii ili kuweka mazingira mazuri ya kufanya biashara na kupata kipato ambacho ni endelevu hata mara baada ya kumalizika kwa shughuli za uchimbaji wa madini.

Ameongeza kuwa mikakati mingine iliyowekwa sambamba na ukusanyaji wa maduhuli ni pamoja na kuhakikisha Sekta ya Madini inakuwa na mchango wa asilimia 10 kwenye Pato la Taifa ifikapo mwaka 2025.

Katika hatua nyingine, Profesa Kikula amesema kuwa Tume ya Madini itaendelea kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wake kwenye utendaji kazi na kuwataka kuendelea kuchapa kazi kwa bidii na weledi na kukidhi matarajio ya wananchi hususan wachimbaji, wachenjuaji na wafanyabiashara wa madini.

Awali akieleza mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa Tume, Profesa Kikula ameeleza kuwa ni pamoja na kuimarika kwa ukusanyaji wa maduhuli kutoka shilingi bilioni 346.78 kwa kipindi cha mwaka 2018-2019 hadi kufikia shilingi bilioni 624.61 kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2021-2022 ikiwa ni sawa na asilimia 96.09 ya lengo la mwaka husika.

Profesa Kikula ameendelea kueleza mafanikio mengine kuwa ni pamoja na uanzishwaji wa masoko 42 na vituo vya ununuzi wa madini 83 na ongezeko la utoaji wa leseni za madini ambapo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021-2022 Tume ilitoa jumla ya leseni za madini 9,498 ikilinganishwa na leseni 6,314 zilizotolewa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020-2021.

Aidha, Profesa Kikula amesema kuwa ili kusogeza huduma karibu zaidi na wadau wa madini, Tume ilianzisha ofisi mpya za madini katika mikoa ya Mbogwe na Mahenge.

Ameendelea kusema kuwa mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa umeendelea kukua kutoka asilimia 4.8 katika kipindi cha mwaka 2018 hadi kufikia asilimia 7.2 katika kipindi cha mwaka 2021.