Site icon A24TV News

SIMANZI JIJI LA ARUSHA WATATU WAFARIKI DUNIA KWA AJALI USIKU SAA KUMI

 

Na mwandishi wa A24Tv

Watu watatu wa familia moja akiwemo mtoto mdogo,wakazi wa kata ya Terat katika jiji la Arusha,wamepoteza Maisha papo hapo kwa ajali baada ya kugongwa na gari wakitoka hospitalini wakiwa wamepakizana kwenye pikipiki.

Tukio hilo la kusikitisha limetokea mapema leo majira ya saa 10.45 usiku katika barabara ya bypass katika jiji la Arusha wakati marehemu wakitoka kumpeleka hospitalini, mtoto Ebenezer Mollel mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu aliyekuwa ameandikiwa sindano za masaa.

Wengine waliofariki dunia ni pamoja na mama wa mtoto ,Neema Mollel(27) pamoja na mdogo wake ,Agustino Mollel (24) ambaye alikuwa dereva wa pikipiki .

Kwa mujibu wa shuhuda wa tukio hilo,John Mushi marehemu hao walipoteza maisha eneo la tukio baada ya kupata majeraha makubwa na kuvuja damu nyingi.

Alisema walishuhudia miili ya marehemu hao wakiwa wamevunjika na kusagika mikono na miguu huku mtoto na dereva wakipasuka kichwa na kusagika.

Naye kaka wa marehemu Daud Mollel alisema kuwa marehemu waligongwa kwa nyuma wakiwa wamepakizana kwenye pikipiki na gari ambalo halikujulikana baada ya kutosimama katika eneo la Karvati ,Terat.

Alisema kuwa mara baada ya kupata taarifa juu ya ajali hiyo alifika eneo la tukio na kushuhudia miili ya marehemu wakiwa ikiwa na majeraha makubwa sehemu mbalimbali za miili yao.

“Marehemu walitoka nyumbani Terat majira ya saa 10 usiku kwenda hospitali ya Murieti baada ya mtoto (marehemu)kuandikiwa sindano za masaa,wakati wakirudi majira ya saa kumi na moja kasoro ndipo walipogongwa na gari kwa nyuma na kufariki dunia”alisema

Kamanda wa polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo alithibitisha tukio hilo na kueleza kuwa bado wanafanya uchunguzi kujua chanzo cha tukio hilo.

Kamanda alisema kuwa gari lililohusika na tukio hilo halikuweza kupatikana na polisi wanaendelea na uchunguzi ili kumtia mbaroni dereva wa gari hilo ambaye alitoweka mara baada ya ajali hiyo.

Miili ya marehemu imehifadhiwa katika chumba cha maiti katika kituo cha afya cha Murieti kusubiri taratibu wa uchunguzi .