Site icon A24TV News

MAKAMU WA RAIS MPANGO ATOA MAAGIZO MAZITO KWA WIZARA NNE

:Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk.Philip Mpango, ametoa maagizo kwa Wizara nne ikiwemo Wizara ya Uchukuzi kupitia wakuu wa mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Uongozi wa uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia), kukaa na kufanya Tathimini ili kuona uwezekano wa kuongeza siku 90 kwa wananchi 1,712 waliovamia eneo la uwanja huo wa ndege.

Hai.Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk.Philip Mpango, ametoa maagizo kwa Wizara nne ikiwemo Wizara ya Uchukuzi kupitia wakuu wa mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Uongozi wa uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia), kukaa na kufanya Tathimini ili kuona uwezekano wa kuongeza siku 90 kwa wananchi 1,712 waliovamia eneo la uwanja huo wa ndege.

Wizara nyingine ni Wizara ya Maji, ambapo imeagizwa kuchukua hatua ikiwemo kuwafukuza kazi watendaji wa bodi na mamlaka za maji nchini, ambao wamekuwa wakiwabambikia wananchi bili za maji na kuwatoza gharama kubwa za maunganisho ya maji majumbani.

Wengine ni Wizara ya Tamisemi ambayo imeelekezwa kufanya tathimini ya shule chakavu zilizopo Wilayani Hai, pamoja na Wizara ya ujenzi kufanya tathimini ya barabara ya Arusha -Holili na upanuzi wa barabara ya Arusha – Moshi, ili iweze kuwekwa kwenye mpango kazi wa utekelezaji kuanzia bajeti ijayo.

Dk Mpango ametoa maelekezo hayo, leo Jumatano, Machi 20,2024, wakati wa uzinduzi wa mradi wa maji wa Kikafu Bomangombe, uliopo Wilaya ya Hai, Mkoani Kilimanjaro ambao umegharimu zaidi ya Sh2.8 bilioni hadi kukamilika kwake.

*Wananchi waliovamia eneo la KIA*

Makamu wa Rais amezungumzia eneo hilo baada ya Mbunge wa Hai, Saashisha Mafuwe, kuomba wananchi kuongezewa siku 90, badala ya 21 walizopewa awali ili kujipanga vizuri kuondoka ikiwemo wengine kumalizia ujenzi wa nyumba zao ambazo wanajenga.

Wananchi hao ambao ni wa vijiji vya Sanya station, Tindigani, Chemka, Mtakuja, Majengo kati, Samaria na Malula wanapaswa kuondoka ndani ya eneo hilo kuanzia Machi 11 hadi Machi 31 ikiwa ni pamoja na kubomoa nyumbani zao, kuondoa mifugo, mazao na usitishwaji wa shughuli zozote za kilimo kwa gharama zao wenyewe.

“Kwa ombi la siku 90 kama ambavyo tayari ilishaelekezwa, Mkuu wa Mkoa na wenzako mkae tena mliangalien muone kama kuna uwezekano wa kuongeza hizo siku 90 kutoka siku 21, hilo tunawaachia tunalimudu.”amesema Dk Mpango na kuongeza kuwa

“Na wale waliotenda mahakamani ndio uhuru wao, hatuwezi kuingulia lakini narudia kusisistiza ni muhimu sana kutafakari vizuri, inapokuja suala la maendeleo la mama Tanzania tushikane mikono na kuacha mambo yetu ya binafsi pembeni”

…….Mimi ninahofia sana, katika viwanja vya ndege tulivyo navyo na viwanja vya ndege vinavyotumika kutuingizia fedha za kigeni ni pamoja na uwanja wetu wa KIA, tuangalie zaidi maslahi ya mama Tanzania,”

Awali, akitoa maombi kwa niaba ya wananchi 1712 wanaotakiwa kuondoka katika eneo la uwanja wa ndege wa KIA, Mbunge wa Hai, Saashisha Mafuwe aliiomba serikali kuongeza siku 90 kwa wananchi hao badala ya siku 21 zilizotolewa na serikali ili waweze kupata muda wa kutosha wa kujipanga kuondoka.

“Ninaomba hawa wananchi waongezewe siku 90 ili waweze kumalizia ujenzi ili waweze kuondoka, zipo changamoto ambazo zipo, ambapo wapo wananchi wamelipwa fidia kidogo, ninaomba rejea ya hawa wananchi waweze kufanyiwa tathmini kulingana na hali halisi, lakini hawa wengine ambao hawajalipwa kulingana na changamoto za kwao wenyewe lakini za kitendaji na zenyewe niombe Makamu wa Rais tusaidie,”

Hata hivyo, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile amesema tayari serikali imeshafanya tathmini kwa wananchi 1,712 ambao wanatakiwa kuondoka eneo hilo la uwanja wa ndege na kwamba mpaka sasa serikali imeshatoa zaidi ya Sh10.3 bilioni kama fidia.

“Mwaka juzi tulianza kufanya tathmini ya maeneo yao, eneo hili linahusisha wilaya ya Arumeru, ambao wanaodai fidia ni watu 681 na 1061 wilaya ya Hai, jumla ni watu 1, 712, na baada ya kufanya uthaminishaji ambao hauhusu ardhi maana eneo lile lilikuwa ni mali ya serikali, uthamini uliunganisha vilivyopo katika ardhi Ile na ilipatikana Sh11.3 bilioni tumeshaanza kulipa na tunalipa kwa awamu 8,”

“Kwasasa tumelipa Sh10.3 bilioni ambapo nisawa na silimia 95 ya malipo yote bado wananchi 81 hawajalipwa fedha zao, katika hawa 81 wapo wananchi 28 ambao hawajalipwa kwasababu mbalimbali lakini wengine mashauri yao yapo mahakamani,”

“Na hili la kuongeza muda wa siku 90,tumefanya mawasiliano serikali pamoja na Wizara, kwa kuwa jambo hili lilipangwa na viongozi wa mikoa hii miwili kwa maana ya Kilimanjaro na Arusha na KIA, sisi tutawaelekeza wakae tena hawa na ushauri watakaoleta tutakuwa tayari kuufanyia kazi kwa lengo la maslahi ya wananchi na kiwanja chetu”

*Ubambikaji Bili za Maji*

Kuhusu wananchi kubambikiwa bili za maji, Dk. mpango alimpa rungu, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kuwachukulia hatua kali ikiwemo kuwafukuza watendaji watakaobainika kufanya hivyo.

“Fukukuza kama kuna watu wanakuzingua, bili za maji wananchi wetu wanalalamila, nataka kutilia mkazo kwamba bodi zote za maji katika Taifa letu, bili za kubambika hapana, Waziri wa Maji wamulike na kuwachukulia hatua mara moja sio kubembelezana tena, saa nyingine peleka vijana huko kimya kimya, kama gharama za kuunganisha maji sio halisia, alafu zinachukua siku nyingi, chukua hatua,”

“Yaani hawa hawa waliokipigia kura chama cha Mapinduzi(CCM) alafu kuungamisha maji zaidi ya siku 7 kwasababu gani?sio serikali ya mama Samia, wachukuliwe hatua,”

Waziri Aweso alisema Wizara hiyo haitakuwa kikwazo kwa wananchi kupata huduma ya maji safi na salama na kuonya bodi na mamlaka za maji nchini kuepuka kuwabambikizia wananchi bili za maji.

Mbali na hilo, Aweso aliagiza maunganisho ya huduma ya maji yasizidi siku saba na gharama ziwe halisi ili kuhakikisha mwananchi ananufaika na matunda ya serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan.

“Tunatambua mradi huu wa Kikafu Bomang’ombe utasimamiwa na bodi ya maji ya Uroki, ninaomba mnisikilize kwa makini, ni haki ya wananchi kupata maji na ni wajibu wa mwananchi kulipia maji”

……..Sasa ni marufuku kuwabambikizia wananchi bili za maji, lakini mradi huu una maji mengi na toshelevu, haitakuwa busara mwananchi anataka kuunganishiwa maji majumbani unamuweka gharama kubwa ya maunganisho anashindwa kuunganisha maji salama”

Akizungumzia mradi wa maji wa Kikafu Bomang’ombe, alisema kwa mujibu wa mkataba, mradi huo ulitakiwa kujengwa kwa gharama ya Sh3.39bilioni lakini umetumia Sh 2.8bilioni hadi kukamilika na zaidi ya Sh500milioni zimebaki.

“Huu ni uzalendo wa hali ya juu nitumie nafasi hii kumpongeza mhandisi wa maji wa Mkoa, Weransari Munisi, na maandiko yanasema ukimaliza kazi utavishwa taji, makamu wa Rais naomba kwa ruhusa yako tumtengenezee zawadi maalum kwa kazi kubwa aliyoifanya”

Alisema “Katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan, anatutoa katika asilimia 54 vijijini mpaka asilimia 79 na asilimia zaidi ya 60 leo tunakwenda asilimia 88, lakini tuna miradi zaidi ya 1,500 inayoendelea maeneo mbalimbali nchini, tumejipanga kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati ili watanzania waweze kupata huduma ya maji safi na salama”.

Meneja wa Ruwasa Mkoa wa Kilimanjaro, Weransari Munisi alisema mradi huo wa maji utanufaisha zaidi ya wananchi 63,049 wa Kata tatu za mji wa Hai na kuondoa tatizo kubwa la maji lililokuwa likiwakabili wananchi wa maeneo hayo na kuongeza kasi ya ukuaji wa maendeleo na uchumi

“Kabla ya mradi huu wananchi wa Mji wa Hai walipata maji kwa asilimia 54 sawa na saa 12 kwa siku ila sasa wanapata maji kwa saa 24 kwa siku, pia utekekezaji wa mradi huu umeongeza upatikanaji wa maji kiwilaya kutoka wastani wa asilimia 89 hadi 92, huku Mkoa wa Kilimanjaro ukifikia wastani wa asilimia 84.5 ya wananchi walioko vijijini wanaopata huduma ya maji safi na salama

*Uchaguzi serikali za mitaa*

Akizungumzia uchaguzi wa serikali za mitaa Dk Mpango amewataka wananchi kote Nchini kuhakikisha kwenye wanawachagua viongozi vijana ambao ni hodari na wenye uchungu na maendeleo ya Taifa.

Hata hivyo, Dk. Mpango aliwaomba viongozi wa dini kote Nchini, kuisaidia serikali katika hilo ili kuhakikisha amani na utulivu unakuwepo katika kipindi cha uchaguzi na kwamba Tanzania ni nchi yetu sote.

“Mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi katika ngazi ya serikali za mitaa, nataka kuwaomba sana wananchi, wananchi wa Hai na wote wa Tanzania chagueni viongozi hodari, viongozi vijana ambao wana uchungu na maendeleo ya maeneo husika,”

“Ndio maana nawaomba mkibahatisha mkamapata kama Saashisha(Mbunge wa Hai) mhakikishe katika ngazi za serikali za mitaa tunapata vijana ambao watakimbiza maendeleo yetu ya wilaya ya Hai,”

…Nawaomba sana viongozi wa dini, katusaidieni katika suala hili la uchaguzi, labda niwakumbushe, mheshimiwa Rais, amekuwa ni kinara wa kukuza demokrasia katika Taifa letu kwa kutambua kwamba Tanzania ni nchi yetu sote,”

“Amefanya na ameongoza maboresho makubwa ndio maana saa hizi jamaa zetu wa vyama vingine wanaandamana na Waziri wa Mambo ya Ndani na vyombo vyake, vimepewa maagizo ya kuwasindikiza wafanye maandamano yao kwa amani, watu watafute haki yao lakini waifanye kwa amani lakini kwa lugha ya staha, tutafute maendeleo ya mama Tanzania,”

Alisema wakati Rais pamoja na wasaidizi wake wakipambana ma demokrasia ya kweli, ili Watanzania wawe na uhuru wa kutoa mawazo yao wanapaswa wakumbuke wanawajibu wa kutunza amani ya mama Tanzania.

“Wakumbuke wajibu wao wa kuijenga nchi, Tanzania haitajengwa na mtu mwingine ni sisi wa Tanzania, nchi haijengwi kwenye mazingira ya vurugu na kwa hili naomba tena viongozi wa dini na kwa wananchi wetu wote, kutunza amani na kuendelea kumwomba Mwenyezi Mungu aijalie nchi yetu amani, na kuchapa kazi.”

*Mirungi*

Akizungumza Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Jumanne Sagini amesema Mkoa huo, hali ya usalama ni nzuri na kwamba mambo madogo madogo yaliyopo ni pamoja na changamoto ya matumizi na usafirishaji wa mirungi pamoja na migogoro ya wakulima na wafugaji.

“Hatuna matukio makubwa ya uvunjifu wa amani maeneo haya, isipokuwa matukio madogo madogo ambayo vyombo vyetu vya usalama vinakabiliana nayo, niombe wananchi waachane na mambo hayo hasa suala la mirungi, haya yapo mkoa wa Kilimanjaro kwenye Wilaya ya Hai, wakiacha hayo hamtasumbuliwa na polisi au Tume ya dawa ya kulevya”

Hata hivyo, Makumu huyo wa Rais alionyesha kusikitishwa na suala hilo na kwamba suala la utumiaji wa mirungi na bhangi linaharibu vijana na kwamba Taifa haliwezi kuwa na vijana ambao kazi yao ni kula mirungi na bhangi.

“Kilimanjaro, suala la kukimbilia mirungi linatoka wapi, nawaomba sana wana Kilimanjaro bhangi na mirungi zinaharibu vijana wetu, sasa mkoa ambao tunategemea tupate Madaktari kama ambavyo imekuwa miaka yote, tupate wataalam, viongozi, nawaomba sana sana na kwenye chama mnapotembelea matawi ya chama viongozi wa dini msisitize sana suala hili la watoto wetu dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya,”

“Tunataka Watanzania vijana ambao wataiendeleza nchi hii na sio vijana mazezeta kazi yao kula mirungi,”alisema Dk.Mpango.

*Soko la kwa sadala,Shule Chakavu*

Kuhusu kukarabatiwa kwa soko la kwasadala lililopo wilayani Hai, Dk.Mpango aliiagiza Ofisi ya Rais-Tamisemi kupeleka Sh11.2 bilioni kwa ajili ya kukarabati soko hilo.

“Maagizo yangu ni kwa Ofisi ya Rais- Tamisemi, hizo fedha Sh11.2 bilioni zije zikafanye kazi ya kukarabati soko hili la kwasadala,”Dk.Mpango

Agizo lingine, alolilitoa ni utekelezaji wa barabara ya kwasadala -lemira kilomita 15 na barabara ya Bomang’ombe-TPC yenye urefu wa kilomita 25.5 ambazo zinatekelezwa na Wakala wa barabara za vijijini na mijini(Tarura) pamoja na Tanroad, ambazo ziliahidiwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

“Nataka kuwakumbusha Tarura, Wizara ya ujenzi na Tanroad kila mmoja ana kipande chake hapa, kipande kimoja ni ahadi ya Rais na najua kilisisitizwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama cha Mapinduzi (CCM),”

“Sasa tupo kwenye mchakato wa bajeti, sitaki kurudi hapa nije wanambie kazi haijaanza, Tarura na Tanroad kila mtu ahangaikie kipande chake, na kwa upande wa Wizara ya ujenzi kuhusu barabara ya Arusha -Holili na upanuzi wa barabara ya Arusha – Moshi, maelekezo yangu mfanye tathminikazi ya upanuzi wa barabara hii iweze kuwekwa kwenye mpango kazi wa utekelezaji kuanzia bajeti ijayo,”

Awali Mbunge Mafuwe, akizungumzia barabara hizo amemuomba Makamu huyo wa Rais kuweka msukumo ili fedha hizo ziweze kutoka mapema kwa ajili ya utengenezaji wa barabara hizo.

 

“Mheshimiwa Makamu wa Rais, barabara ya Kwasadala- Lemira kilomita 15 tunakuomba sana mheshimiwa barabara hii ishafanyiwa upembuzi yakinifu, katusaidie kusukuma tupate fedha hili ni muhimu sana,”

Alisema barabara nyingine ambayo ni ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa wananchi wa Hai ni barabara ya Bomang’ombe-TPC ambapo ndipo kilipo chanzo cha maji cha chemka.

Pamoja na mambo mengine, Mbunge Mafuwe amesema Wilaya hiyo ina shule nyingi za msingi na Sekondari na kwamba shule nyingi ni chakavu.

“Rais alikuja hapa nikamwomba na akaniahidi lakini naomba na wewe hili ulibebe shule hizi zinahitaji fedha maalum, tunaomba itusaidie ili sisi tuendelee kuchapa kazi,”

Akijibu suala hilo, Makamu huyo wa Rais amesema “Ofisi ya Rais- Tamisemi nawataka pia mfanye tathmini ya hizi shule ambazo nimeambiwa zimechakaa, Rais amefanya kazi kubwa sana kujenga shule nzuri nchi nzima, mfanye tathmini ili shule hizi ziweze bora na nzuri kama zilivyo shule nyingine za mama Samia,”

Mwisho.