Site icon A24TV News

MAADHIMISHO YA SIKU YA WANAWAKE, MANYARA YATUMIKA KUKEMEA UKATILI WA KIJINSIA NA MAUAJI.

Na John Walter-Babati
Shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na utoaji elimu ya utunzaji wa Mazingira na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia wilaya ya Babati (BAMBAGO FOUNDATION) wamesherehekea siku ya wanawake duniani kwa kutoa elimu katika maadhimisho yaliyofanyika tarafa ya Bashnet kata ya Madunga Halmashauri ya wilaya ya Babati.
Akizungumza na wananchi hao mratibu wa BAMBAGO FOUNDATION Lucy Sylvester, aliwasihi wananchi kuripoti vitendo vya UkatiliĀ  vinapotokea katika maeneo yao na kuwa Karibu na watoto wao.
Mratibu aliambatana na katibu wa Shirika hilo wilaya ya Babati Deogratius Gwasma ambaye alifafanua kuwa suala la Vitendo vya Ukatili wa Kijinsia vimekuwa tishio kubwa wilayani humo na kufifisha ndoto za Wanafunzi kwa kupewa ujauzito,kubakwa hadi kufa, baadhi ya wanume kuwaua wake zao kwa wivu wa mapenzi.
Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) wilaya ya Babati nao waliungana na taasisi zingine za serikali na binafsi kutoa elimu juu ya Ukatili wa kijinsia.
Simon Gervas kutoka shirika binafsi linalojishughulisha na masuala ya afya la Thrive Afya Tanzania amesema wanawake ni jeshi kubwa na lazima waheshimiwe na kulindwa dhidi ya ukatili kwa nguvu zote.
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Babati Anna Mbogo ameguswa na tukio la mauaji lililotokea februari 17, 2024 katika kata ya Madunga, ambapo mwanaume mmoja ambaye hadi sasa jeshi la polisi linaendelea kumtafuta, alimuua mkewe akiacha watoto saba.
Mkurugenzi alichangisha shilingi 6,94,550 kwa ajili ya kuwasaidia watoto wa marehemu ambao wanasoma katika shule ya msingi Lakita kwa msaada wa Msamariawema.
Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Babati Mjini Mheshimiwa Jackson Buu Hhaibei ameataka wanaume kuwa mstari wa mbele kupinga ukatili ili jamii iwe salama kwa watu wote.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Manyara Queen Sendiga ambaye aliungana na wanawake kusheherekea siku ya wanawake duniani katika uwanja wa Tanzanite Kwaraa, amewasihi wanawake kutumia fursa za mikopo inayotolewa na serikali na taasisi za kifedha katika kuendeleza biashara zao na kuepuka kutumia mikopo hiyo kufanya mambo ambayo hayana tija.
Kauli mbiu siku ya wanawake duniani mwaka 2024, Wekeza kwa Mwanamke kuharakisha Maendeleo ya taifa na ustawi wa Jamii.