Site icon A24TV News

WAZIRI MKENDA AWATAKA WAHITIMU ADEM KUWA VIONGOZI WA MAGEUZI YA ELIMU

Na Mwandishi wa A24tv .

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema Serikali inawatarajia Wahitimu katika mafunzo ya elimu kuwa mabalozi wa utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 Toleo la 2023.

Prof. Mkenda ametoa rai hiyo Disemba Mosi, 2023, Bagamoyo Mkoa wa Pwani wakati akizungumza kwenye mahafali ya 31 ya Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM).

“Katika kipindi hiki, tunawategemea sana kwenda kutusaidia kutekeleza mageuzi ambayo yameanishwa katika Sera mpya ya Elimu, pamoja na jukumu la kufundisha mtaenda kusimamia mabadiliko ya elimu nchini” Alisema Prof. Mkenda.

Amesema Serikali imeanza mchakato wa mabadiliko ya Sheria ya elimu ya mwaka 1978, na kwamba kulingana na Sera Mpya ya elimu ma Mafunzo, elimu ya lazima miaka 10 badala ya miaka 7.

“Kutokana na mabadiliko ya Sera tunapitia sasa sheria ya elimu ya mwqla 1978 ili iendane na sera pamoja na masuala mengine muhimu, mtambuka” Alieleza Waziri Mkenda.

Mkenda ameongeza kuwa katika Sera na Mitaala Mipya walimu watapaswa kufanya mafunzo kwa vitendo kwa muda wa Mwqka mmoja ili kujenga uzoefu kazini na kueleza kuwa matarajio ni kuwa wahitimu wq Ualimu na Uthiviti Ubora wa Shule wakiwa kazini Serikqli na jamii inawategemea sana katika kufundisha na kuwalinda wanafunzi na si viginevyo.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) Dkt. Siston Masanja amesema serikali inawekeza katika mafunzo hayo ili kuwajengea Walimu umahiri na uwajibikaji kwa Maendeleo ya nchi, hivyo wanapaswa kuwa imara na mawazo chanya katika kusimamia Shule ili kuleta mageuzi chanya yanayokusudiwa.

“Wahitimu ni nguzo muhimu ya taifa, mnapaswa kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa miradi ya ujenzi, usimamizi wa ufundishaji na ujifunzaji, kuzingatia usalama wa watoto pamoja na miongozo mbalimbali” alisema Dkt. Masanja.

Ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kutoa fedha zinazosaidia kutekeleza ujenzi wa Kampasi ya ADEM Mbeya.

Jumla ya Wahitimu 916 wametunukiwa Stashahada, Wahitimu 702 ni wa kozi ya Stashaha ya Uongozi na Usimamizi wa Elimu (DEMA), 214 Stashahada ya Udhibiti Ubora wa Shule (DSQA) na wahitimu 03 wametunukiwa Astashahada ya Uongozi na Usimamizi wa Elimu (SELMA).

Mwisho .