Site icon A24TV News

NAIBU WAZIRI KIKWETE ,AZUNGUMZA NA WATUMISHI WA CHUO CHA UFUNDI ARUSHA; KUHUSU MIFUMO YA UPIMAJI UTENDAJI KAZI

Na Mwandishi wa A24tv .

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma, Menejimenti na Utawala Bora Mhe. Riziwani kikwete amesema kuwa Serikali imeboresha mifumo ya upimaji utendaji kazi kwa watumishi wa Umma ambayo itawezesha watumishi kutekeleza majukumu yao waliyopangiwa ipasavyo na kurahisisha kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi.

Mhe. Kikwete amesema hayo wakati akizungumza na watumishi wa wa Chuo cha Ufundi Arusha, wakati watumishi hao wakiwa kwenye mafunzo ya mifumo ya PEPMIS na PIPMIS yaliyofanyika kwenye ukumbi wa chuo hicho.

Amesema kuwa mifumo hiyo imekuja kutokana na maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye alielekeza aina ya utumishi wa Umma unaohitajika na kutambua kwa urahisi namna watumishi wanavyotekeleza majukumu yao ya kila siku baada ya mfumo wa awali uliokuwa unatumika wa OPRAS kuonekana kuwa na mapungufu kadha wa kadha.²

“Mifumo hii ni muhimu sana kwa Serikali kutambua watumishi ambao hawawajibiki kwenye majukumu yao sambamba na kupata mrejesho wa utendaji kazi kupitia uwasilishaji wa taarifa kila baada ya muda flani, hivyo niwatake mzingatie yale mtakayofundishwa kwa manufaa ya Taifa zima kwa ujumla”. Amesisitiza Mhe. Kikwete.

Kwa upande wake katibu Tawala Msaidizi Utawala na Rasilimali Watu, David Lyamongi amesema kuwa zoezi hilo la kutoa mafunzo hayo linaendelea vizuri mkoani humo kwa wakuu wa Taasisi zenye makao makuu mkoani humo pamoja na wakuu wa Idara za Utumishi na Utawala bora.

Hata hivyo, Mkuu wa chuo hicho Dkt. Mussa Chacha ameahidi kuendelea kushirikiana na wataalam wanatoa mafunzo hayo ili kuhakikisha yanaleta manufaa huku akikiri kuwa mfumo huo utarahisisha upimaji utendaji kazi wa kila mtumishi kwa haki.

 

Mwisho .