Site icon A24TV News

MABARAZA YA WAHITIMU NI CHACHU YA MAENDELEO VYUO VIKUU PROF. MKENDA

Na Mwandishi wa A24Tv Morogoro

Waziri wa Elimu, Sayansi na teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema serikali inatambua umuhimu wa Mabaraza ya Wahitimu na Jumuiya mbalimbali katika Vyuo Vikuu, katika kuchangia Maendeleo ya miradi mbalimbali katika Vyuo husika.

Prof. Mkenda ametoa kauli hiyo Novemba 22, 2023 mjini Morogoro wakati akihutubia Baraza la Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe ambapo amesema serikali inajivunia michango ya Wajumbe wa Baraza hilo, ikiwemo mchango wa ujenzi wa mabweni kwa ajili ya Wanafunzi Ndaki ya Mbeya.

“lakini pia nawapongeza kufikia katika hatua za mwisho za kuanzisha mfuko wa ufadhili kwa ajili ya kusaidia wanafunzi wasio na uwezo kugharamia masomo, na kwamba Sera ya mfuko huo tayari imeandaliwa na kupitishwa na ngazi husika nawapongeza sana na ninaamini katika utoaji ufadhili mtazingatia pia _meritocracy_ ” alisema Prof. Mkenda.

Wakati huo huo Prof. Mkenda amekipongeza Chuo hicho kwa kuanzisha kituo cha Mafunzo ya Uongozi na Menejimenti na kwamba hatua hiyo inaashiri kurudisha mafunzo kulingana na madhumuni halisi ya Chuo ya kuandaa na kutoa elimu ya Uongozi katika ngazi mbalimbali.

“Ni muhimu Chuo Kikuu Mzumbe, kupitia kituo hiki, muendelee na utamaduni wa kutoa huduma ya kuwajengea uwezo viongozi wetu, hasa kwenye ngazi za kati na chini” alisema Prof. Mkenda

Awali akitoa taarifa kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mkurugenzi wa Elimu ya Juu Prof. Peter Msofe ameeleza kuwa Wizara inaona umuhimu mkubwa katika kudumisha uhusiano wa karibu na Mabaraza ya Wahitimu wa Vyuo Vikuu katika kusimamia dhana ya elimu ya juu nchini.

“Tunatambua kuwa Vyuo Vikuu ni nguzo muhimu katika Maendeleo ya taifa letu, na ndio maana tunajitahidi sana kuhakikisha tunashirikiana kuweka mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia” alieleza Prof. Msofe.

Nae Rais wa Baraza la Wahitimu katika Chuo Kikuu Mzumbe CPA. Ludovick Utoah ameipongeza serikali kwa kuendelea kusimamia mageuzi makubwa yenye mchango chanya katika sekta ya Elimu kwa kuzingatia viwango vya juu.

“Kazi inayofanya Wizara ya elimu, ambayo sisi ni wadau tunaithamini sana hasa kwa namna inavyotekeleza mipango mbalimbali katika sekta ya Elimu, Sayansi na teknolojia Kwa niaba ya Mhe. Rais.

Mkuu wa mkoa wa Morogoro mhe. Adam Malima amemshukuru Rais Mhe. Samia kuendelea kufanya uwekezaji kwa kuboresha mbiundombinu ya elimu katika Vyuo Vikuu ikiwemo Chuo Kikuu cha Mzumbe ambacho kimekuwa kinara katika kuzalisha Wataalam katika masuala ya uongozi.

Aidha Mkuu huyo wa Mkoa ameipongeza Wizara ya elimu katika kusimamia mabadiliko makubwa ya elimu yanayolenga kuwezesha kutoa elimu inayojenga ujuzi kwa Wahitimu katika ngazi mbalimbali

“Nawapongeza kwa namba mnavyomsaidia Mhe. Rais kusimamia vema mageuzi ya elimu nchini, nimeona kazi kubwa iliyofanyika katika maboresho ya Sera ya elimu na Mitaala hii itawezesha kuinua kiwango cha elimu, ” Alisema Mhe. Malima.

Akitoa taarifa kuhusu utekelezaji wa miradi na shughuli mbalimbali za kitaaluma Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Prof. William Mwegoha amesema Chuo hicho kinaendelea kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji pamoja na kuhuisha mitaala iweze kuakisi mabadiliko makubwa yanayotarajiwa katika taifa hilo.

“Tunatambua mageuzi haya yanaakisi malengo ya serikali ya awamu ya Sita ambayo inasisita umuhimu wa Elimu inayotolewa katika ngazi zote nchini, kukidhi mahitaji ya jamii katika taifa letu” amebainisha Prof. Mwegoha

Mwisho