Site icon A24TV News

Atakayekwamisha Wafanyabiashara ni adui namba moja wa Serikali

Na Mwandishi wa A24Tv .

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah amesema Afisa yeyote wa Serikali atakayekwamisha ufanyaji biashara, uwekezaji au uanzishwaji viwanda nchini ni adui namba moja wa Serikali na atachukuliwa hatua za kisheria.

Vilevile, Ametoa wito kwa watendaji hao kuwezesha uwekezaji, ufanyaji biashara, uanzishaji viwanda na kuhakikisha kila mwekezaji anapata anachostahili kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo.

Dkt. Abdallah ameyasema hayo Septemba 25, 2023, wakati akiongoza Kamati Maalum ya Katibu Mkuu Kiongozi inayojumuisha Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Fedha, Mipango na Uwekezaji, Kilimo na Katibu Tawala Mkoa wa Kagera walipotembelea Kiwanda hicho kuona hali ya uwekezaji na kutatua changamoto walizonazo.

Aidha, Dkt. Abdallah amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan ameweka Sera na Mazingira wezeshi katika ufanyaji biashara uwekezaji na uanzishaji wa viwanda ili kuiwezesha Tanzania kujitosheleza katika mahitaji ya bidhaa muhimu na kuuza ziada nje ya nchi na kutimiza malengo ya Tanzania kuilisha Dunia.

Akifafanua zaidi, Amesema Serikali imeanza kutimiza malengo hayo kwa kuanza na Sekta ya Sukari ambapo Kiwanda cha Sukari cha Kagera kinauwezo wa kizalisha tani 150,000 kwa mwaka katika 2023/2024 na kinapanga kizalisha tani 300,000 kwa mwaka kitakapokamilisha upanuzi wa awamu ya nne na hivyo kuchangia kuifanya Tanzania kutokuagiza sukari nje ya nchi, kuongeza ajira na pato la taifa hususan fedha za kigeni.

Naye Katibu Tawala Mkoa wa Kagera Bw. Tobi Nguvilo amesema uongozi wa Mkoa huo uko tayali kumlinda, kumtunza, kumsaisia na kuhakikisha hakwami kwa jambo lolote Mwekezaji wa Kiwanda cha Sukari cha Kagera kwa kuwa Mkoa huo unakitegemea kiwanda hicho kwa ukuaji wa uchumi na maendeleo ya kijamii kwa kuajiri wananchi 115,000 kutoka Mkoani humo pamoja na utoaji wa huduma bora za shule na hospitali.

Vilevile, Mwenyekiti wa Chama cha Wazalishaji Sukari na Mmiliki wa Kiwanda cha Sukari Kagera Bw.Self Ally Seif amesema anaungana mkono juhudi za Serikali kwa katika kuwawezesha wawekezaji ili kitimiza dhamira ya kuiwezesha Tanzania kuilisha Dunia kwa kuanza na Sekta ya Sukari inayotoa ajira nyingi na kuongeza pato la taifa zikiwemo fedha za kigeni.

Mwisho.