Site icon A24TV News

JAMII ZA PEMBEZONI KUTUMIA NJIA ZA ASILI KUTATUA MIGOGORO

JAMII za pembezoni hapa nchini hasa za kifugaji zimetakiwa kutumia njia za asili wanazotumiaga kila siku kutatua migogoro mbalimbali katika jamii.

Rai hiyo,ilitolewa jana jijini Arusha na Rose Njilo,Mratibu wa Shirika la MIMUTIE WOMEN ORGANIZATION(MWO),wakati wa maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Watu wa asili duniani ambayo yaliratibiwa na shirika hilo.

Alisema kuanzia Januari mwaka huu wamefanikiwa kuwanusuru watoto 11 ambao walikuwa tayara kuozeshwa kwenye umri mdogo.

Hata hivyo,alisema shirika hilo,limefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa asilimia 75 kupambana na ukatili wa kijinsia kwa watoto na wanawake hasa kupambana na ndoa za umri mdogo na mimba za utotoni.

“Kama taasisi tumekuwa tukipokea kesi mbalimbali ikiwamo za wanawake kunyanganywa ardhi kwa kuwa ni wajane au kutopata mtoto wa kiume,lakini pia kabla ya kuanzisha kituo hiki masurusa wa ukatili waliporipotiwa tulikosa sehemu salama za kuwapeleka.

Vilevile alisema wamefanikiwa kuwasaidia watoto wakike ambao wengi wao kwa sasa wako shuleni wanasoma kwa ngazi mbalimbali za elimu ili kufikia malengo yao.

“Vyombo hivyo vya asili ni pamoja na viongozi wa kimila kwa (Laigwanani) na (Ingaigwanak) kwa wanawake kupaza sauti na kuondoa na kutokomeza mil azote kandamizi.

Naye Iddi Ninga,kutoka katika Mtandao wa Mashirika ya Kupinga Ukatili wa Kijinsia katika Jamii za Pembezoni,alisema katika kuadhimisha siku hiyo,wametoka na mapendekezo mbalimbali ambayo yakitumika yatasaidia kutokomeza ukatili. huo.

Alisema kuna mbinu mbalimba za asili ambazo zinakwenda sambamba na utamaduni kwenye jamii hizo,kwa kuwa zikitumika vema zinaweza kuwa msaada wa kutokomeza ukatili huo.

Neema Laizer,mkazi wa Simanjiro mkoani Manyara,akisoma taarifa fupi kwenye maadhimisho hayo,aliomba serikali kutambua sheria na hukumu za viongozi wa kimila kama sheria za asili ili kutatua migogoro bila ya kuathiri za nchi.

Pia alipendekeza kuwapo na shughuli za kitamaduni za kuhamasisha kupinga ukatili wa kijinsia ikiwamo ‘Alamal’ kadhalika mila kandamizi na uongozi ziwe mila shirikishi kwa wanaume na wanawake ili kuweka usawa wa kijinsi.

“Tunaomba serikali, ili itambue kisheria na kisera jamii hizi asili pamoja na maeneo yao kwa kuwa wanawake na watoto wapate utulivu na maendeleo,lakini pia serikali iweke huduma muhimu za kibinadamu katika jamii za asili,”alisema.

Mwisho