Site icon A24TV News

TUME HAKI ZA BINADAMU YAWEKA BAYANA KIFO CHA NUSURA.

Na Doreen Aloyce,Dodoma

Kufuatia kifo cha aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) Marehemu Nusura Hassan ABdallah Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imetoa matokeo ya uchunguzi wa Kifo chake na kidai kwamba kilitokana na Kisukari

Taarifa hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Tume hiyo ,Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu wakati alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari Jijini Dodoma na kusema kuwa kazi ya uchunguzi wa kifo hicho umekamilika kwa mujibu wa Kifungu cha 15(1)(a) cha Sheria ya THBUB, Sura ya 391, kinachoipa uwezo wa kuanzisha uchunguzi.

Ambapo katika uchunguzi huo Jaji Mstaafu Mwaimu amebainisha maeneo yoye yaliyohisishwa kwenye taarifa za awali zilizokuwa zikisambaa katika mitando ya kijamii ikiwemo kifo hicho kuhusishwa na ajali ya gari iliyomhusu Mhe. Dkt. Festo John Dugange (Mb), Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – OR, TAMISEMI (Afya).

Katika uchunguzi huo, THBUB ilitembelea eneo ilipotokea ajali ya gari iliyomhusisha Mhe. Dkt. Dugange; nyumbani kwa Mhe. Dkt. Dugange; Kituo cha Polisi (Traffic) Mkoa wa Dodoma; Hospitali ya Benjamin Mkapa; na Chuo Kikuu cha Dodoma,”

Na kuongeza “Pia,THBUB ilitembelea Kijiji cha Mandewa, Kata ya Mandewa, Wilaya ya Singida Mjini wanakoishi wazazi wa marehemu Nusura Hassan Abdallah; Kitongoji cha Mtakuja Kijiji cha Kikonge, Wilaya ya Iramba alikozikwa Nusura; Ofisi ya Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro; Hospitali ya Faraja iliyopo Himo, Mkoa wa Kilimanjaro; na maeneo mengine kwa madhumuni ya kupata maelezo ya watu mbalimbali kuhusu ajali ya Naibu Waziri na mazingira ya kifo cha Nusura Hassan Abdallah,” ameeleza Jaji Mstaafu Mwaimu.

Aidha Daktari aliyempatia huduma na ndugu wa marehemu walioutayarisha mwili kwa ajili ya mazishi na kuuona mwili huo kabla ya mazishi walithibitisha kuwa haukuwa na dalili za kupigwa, kujeruhiwa wala majeraha;

Mabaki ya chakula walichokula Marehemu Nusura, mchumba wake na mpwa wa mchumba wake; na matapishi yaliwasilishwa katika Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi, na baada ya kufanyiwa uchunguzi taarifa ilionesha kutoonekana kwa dalili yoyote ya kuwemo kwa sumu;

Gari iliyopata ajali ilikuwa ni gari binafsi aina ya Toyota Land Cruiser GXR V8 yenye namba za Usajili T454 DWV, iliyokuwa ikiendeshwa na Mhe. Dkt. Festo Dugange, Naibu Waziri, OR – TAMISEMI (Afya). Naibu Waziri alikuwa peke yake katika gari hilo;

Kutokana na mazingira hayo, THBUB imebaini kuwa kifo cha Marehemu Nussura Hassan Abdallah hakikuwa na uhusiano wowote na ajali ya gari aina ya Toyota Land Cruiser GXR V8 yenye namba za usajili T454 DWV iliyomhusisha Mhe. Dkt. Festo John Dugange, Naibu Waziri TAMISEMI (Afya) iliyotokea usiku wa tarehe 25 kuamkia tarehe 26 Aprili, 2023 katika eneo la Iyumbu, jijini Dodoma;

THBUB haikuweza kuthibitisha mtu yeyote kuhusika na kifo cha Marehemu Nusura Hassan Abdallah kutokana na vielelezo vya Hospitali ya Faraja, Mkemia Mkuu wa Serikali, na maelezo ya mengine ya mashahidi;

THBUB inatambua hatua zinazoendelea kuchukuliwa na vyombo vingine ikiwemo Jeshi la Polisi Tanzania na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka katika kulishughulikia suala hili kijinai.

JE NINI MAPENDEKEZO YA TUME

Kuwa Jeshi la Polisi Tanzania na mamlaka nyingine zichukuwe hatua ili kuwabaini wale wote wanaohusika na kutoa taarifa za uongo na chonganishi zinazosababisha taharuki katika jamii;

Jeshi la Polisi Tanzania kwa kushirikiana na mamlaka za usafiri barabarani liweke vifaa vya kiusalama barabarani kama vile kamera ili kubaini (detect) matukio yanayotokea barabarani huku
Wananchi waepuke kutoa taarifa zinazoweza kuchochea chuki na kusababisha uvunjifu wa amani;

Wananchi waendelee kuwa na imani na vyombo vya dola katika kuzuia na kupambana na uhalifu na watoe ushirikiano katika kuvisaidia vyombo hivyo kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Mwisho.