Site icon A24TV News

Waziri Mkuu Mgeni Rasmi Mkutano wa Mawaziri wa Michezo Nchini 14 Afrika

Na Geofrey Stephen Arusha

Tanzania imeomba kuwa Makao Makuu ya kudumu ya Kamati ya Baraza la Wataalamu wa Michezo Kanda ya IV Afrika lengo ni kutaka kuboresha zaidi sekta michezo katika Ukanda huo.

Hayo yalisemwa leo{jana} na Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni,Michezo na Sanaa,Said Yakubu wakati akifungua Kikao cha kamati hiyo ambapo wajumbe wake ni Wakurugenzi wa Michezo katika Nchini 14 za Ukanda wa IV Afrika .²

Yakubu alisema kuwa Tanzania imewasilisha rasmi ombi kwa kamati hiyo la kutaka Makao Makuu ya kamati hiyo yawe hapa Nchini na  Tanzania ina sifa na vigezo vyote kwa kamati hiyo Makao yake kuwa Arusha Jiji lenye sifa ya Geneva ya Afrika.

Alisema moja ya sifa ya Tanzania ni pamoja na kuwa na Diplomasia ya Michezo,Tanzania inaboresha Miundombinu ya Michezo na sekta ya Michezo inakuwa katika ukanda huo hususani katika soka la wanawake kwa umri zote.

Katibu Mkuu huyo alisema kuwa Kamati hiyo ya Wataalamu imeshaanda katiba ambayo inatarajiwa kupata baraka na Mawaziri wa michezo,Utamaduni na Sanaa kutoka katika Nchi hizo 14 za Ukanda wa IV Afrika.

Alisema mbali ya hilo kamati hiyo imeboresha uendeshaji wa kamati hiyo ili iweze kwenda na wakati lengo likiwa kukuza michezo yote katika ukanda wa IV Afrika tofauti na zamani.

Yakubu alisema katika Mkutano wa Mawaziri wa Michezo ,Utamaduni na Sanaa wa Nchi 14 za ukanda wa IV wa Afrika unaotarajia kufanyika kesho,Waziri Mkuu Kassimu Majawaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Alisema Mkutano huo Mara ya mwisho ulifanyika Nchini Uganda mwaka 2018 kabla ya kuzuka kwa ugonjwa wa COVID 19 na sasa unafanyika hapa Nchini hususani katika Jiji la Arusha na wageni zaidi ya 300 kutoka Ukanda huo wanakutana.

Alisema Baraza hilo ni chombo cha Umoja wa Afrika{AU} kinachoshughulikia michezo na kuna kanda nyingine mbalimbali ndani ya Baraza hilo zinazojumuisha Nchi nyingine ambazo ni wanachama wa AU.

Alisema na kuzitaja Nchi 14 ni pamoja na wenyeji Tanzania ,Kenya,Uganda,Rwanda,Ethiopia,Sudan,South Sudan ,Eritrea ,Somalia ,Djibout ,Mauritius ,Madagascar ,Comoro na Seychelleys na hadi jana Nchi nane zimeshathibitisha kushiriki Mkutano huo.

Yakubu alisema katika Mkutano huo pia viongozi wa Mashirikisho ya vyama vyote vya michezo watashiriki Mkutano huo,Viongozi Wakuu wa Baraza la Michezo Nchini{BMT} na Viongozi wakuu wa Baraza la Michezo Zanzibar{BMZ} na Waziri wa Utamaduni,Michezo na Sanaa Zanzibar pia atashiriki.

Alisema pia Viongozi wa vyama vya soka vya Nchi za Kenya na Uganda nao wamealikwa katika Mkutano huo lengo ni kutaka kila nchi za EAC kushiriki kikamilifu Mkutano huo.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo Nchini,Ally Mayai alisema kuwa agenda kuu ya Mkutano wa Kamati ya wataalamu wa Michezo Ukanda wa IV Afrika ni kupitisha mapendekezo ya katiba kabla ya kubarikiwa na  Mkutano Mkuu wa Baraza la Mawaziri Michezo wa Ukanda huo unaotarajiwa kufanyika kesho Jijini Arusha.

Mayai alisema kupitishwa kwa katiba hiyo itaongeza ushirikiano katika sekta ya Michezo na Mataifa mengi yameendelea kwa sababu ya ushirikiano kwa kujenga na kusimamia mpango kazi wa Maendeleo ya Ukanda huo.

Alisema baadhi ya wajumbe katika Mkutano huo wamesema kuwa Tanzania katika ukanda wa IV Afrika inaongoza kwa wananchi na wataalamu wenye kupenda michezo.

Mwisho