Site icon A24TV News

WAZIRI MKUU AZITAKA NCHI ZA UMOJA WA AFRICA KUKUZA MICHEZO NA KUZITANGAZA KIMAITAIFA

Geofrey Stephen Arusha

WAZIRI Mkuu, Kassimu Majaliwa amezitaka Nchi za Umoja wa Afrika(AU) wa Baraza la Michezo Ukanda wa IV Afrika kushikamana na kushirikiana katika kukuza michezo lengo likiwa kuitangaza Kanda hiyo Kimataifa katika fani za michezo mbalimbali.

Majaliwa amesema hayo leo wakati akifungua Mkutano wa Mawaziri wa Michezo ,Utamaduni na Sanaa wa Nchi 14 za Afrika Ukanda wa IV uliofanyika Jijini Arusha na kusema kuwa njia pekee ya kukuza michezo ni kwa nchi hizo kushikamana na kushirikiana kwani hakuna mafanikio ya njia ya mkato katika kuendeleza soka

Alisema Ukanda wa IV Afrika katika kukuza michezo Inawezekana na siri ya kukuza michezo ni kushirikiana kwa nchi zote za ukanda huo na nchi yoyote ikiwa inafanya vizuri katika mchezo fulani Basi unapaswa kuungwa mkono kwa dhati.

Waziri Mkuu amesema kila mmoja au kila nchi awekeze katika kujenga uwekezaji katika uwekezaji wa michezo na kupiga vita kushika mkia katika mashindano hivyo ni wajibu kuweka mikakati ya pamoja kukuza michezo katika ukanda huo.

Alisema ifike wakati kila nchi iwe na tabia ya kuunga mkono nchi itakayofanya vizuri katika michezo hiyo itatia morara kwa nchi za ukanda mwingine kuiga mfano wa Ukanda wa IV.

” Tunahitaji kushikamana na kushirikiana katika fani ya michezo na mshikamano huo uweze kuigwa na kanda nyingine za Afrika na ikiwezekana tuweze kufanya vizuri katika michezo ngazi ya Dunia” alisema Majaliwa

Mbali ya hilo aliwaomba Mawaziri hao wa michezo wa ukanda huu kukubali ombi la Tanzania kuwa Makao Makuu ya Sekretarieti ya Baraza la Michezo la Ukanda wa IV Afrika kwani Tanzania Ina sifa za kuwa Makao Makuu ya Sekretarieti kwa kuwa fani ya michezo mbalimbali hapa Nchini imekuwa ikikua siku hadi siku na imezidi kuileta sifa nchi.

“Tuna sifa za kuwa Makao Makuu ya Sekretarieti ya Baraza la Michezo la Afrika Ukanda wa IV hivyo tunaamini Mawaziri wa Michezo wa Nchi 14 Afrika kuipa Tanzania Kura na kuwa Makao Makuu ya Sekretarieti” alisema Majaliwa.

Naye Waziri wa Utamaduni ,Michezo na Sanaa,Dk Pindi Chana kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu alisema kuomba Tanzania kuwa Makao Makuu ya Sekretarieti ya Baraza la Umoja wa Afrika Ukanda wa IV ni mwendelezo wa maono ya watangulizi wake yanayothibitisha utayari ambao serikali inao na kujipanga kutoa huduma stahiki kwa mafanikio ya sekta ya michezo kwa Mataifa yote ya Ukanda IV.

Dk chana alisema kuwa mkutano huo wa siku moja wa mawaziri utakuwa na agenda maalum zinazolenga kutoa mwelekeo na mstakabali wa sekta ya michezo kwa nchi wanachama wa Ukanda wa IV na moja ya agenda mahsusi ni pamoja na mkutano huo kupitisha mpango kazi wa baraza na mawaziri kupitisha makao makuu ya sekretarieti ya baraza hilo.