Site icon A24TV News

NAMELOK SOKOINE ASHINDA UNEC, HUSSEN GONGA NITASHIRIKIANA NAE UCHAGUZI ULIKUA HURU NA HAKI

Na Geofrey Stephen ,Arusha

Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa Arusha wamemchagua Namelok Sokoine kuwa Mwakilishi wa Mkoa huo katika nafasi ya NEC Mkoa Kuwasilisha Chama hicho Taifa.

Akitangaza Matokeo hayo,Waziri Mkuu Mtaafu,Mizengo Pinda alimtakaza Sokoine kwa kuongoza na kupata kura 39 na kumwangusha mpinzani wake wa karibu Mfanyabiashara Hussein Gonga aliyeambulia kura 16.

Pinda alisema kuwa wajumbe waliopiga kura walikuwa 67 na nafasi ya tatu Daniel Palangyo aliyetetea nafasi ya NEC kwa kupata kura 5,nafasi ya Judith Mollel alipata kura 3,Elibahati Lowassa na David Lemilla walioambulia kura 2 na wagombea wengine Novatus Makunga,Prf Samweli Ilila na Abdullazi Mawia walioambulia kura sifuri

Pinda ambaye alikuwa mfanyakazimlezi wa CCM Mkoa Arusha aliwataka wajumbe kumpa ushirikiano Namelok katika kuifanya kazi yake vizuri na kuacha kumvua shati kwani hiyo sio stahili ya uongozi ndani ya chama.

Namelok amewataka Wana CCM kuvunja Makundi kwani CCM ni moja na kundi lililobaki ni moja la chama Cha Mapinduzi na sio vinginevyo.

 

Gonga aliwashukuru viongozi wa chama kwa jinsi walivyoendesha uchaguzi wa wazi na huru na Yale yote aliyotaka kuyafanyia kazi iwapo angeshinda Sasa atapeleka kwa Namelok na atashirikiana naye kwa Hali na Mali.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha Zelothe Stephen aliwataka wana CCM kumpa ushirikiano Sokoine na kusema kuwa kilichobaki ni kuijenga CCM na sio vinginevyo.

Mbunge wa Jimbo la Arusha,Mrisho Gambo alipopewa nafasi ya kusalimia alionyesha wazi kukerwa na namna anavyoshughulikiwa na uongozi wa serikali Mkoa,Wilaya na serikali ngazi hiyo na kusema kuwa yeye ataendelea kukitumikia chama kwani ndio waliompa nafasi ya kuwa mbunge.

Hata hivyo hoja hiyo ilionekana kupingwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa na kusema kuwa mwenye malalamiko ndani ya chama anapaswa kufuata taratibu kwani hoja iliyopo mbele ya Mkutano huo ilikuwa uchaguzi wa mjumbe wa NEC Mkoa wa Arusha na sio vinginevyo.

Mwisho