Site icon A24TV News

WAZIRI MKENDA AZINDUA MKOPO WA ELIMU KUTOKA BENK YA NMB.

Na Doreen Aloyce, Dodoma

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda ametoa wito kwa wadau mbalimbali kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutoa elimu nchini.

Waziri Mkenda ametoa wito huo jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa huduma ya mkopo wa Elimu inayotolewa na Benki ya NMB.

Amesema kinachofanyika na Benki ya NMB ni kuonyesha njia kwa kuwa pamoja na kuanzisha mkopo wa elimu wamekuwa wakitoa ufadhili wa masomo ambapo kwa mwaka huu wamenufaisha wanafunzi 100.

“Mwaka jana Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB alikuja ofisini kwangu akasema tunataka kuunga mkono juhudi za Serikali na tunachagua eneo ambalo Mhe Rais ameelekeza nguvu kubwa kwa kutenga Sh bilioni 200 na kwa kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 100 na leo ni siku ya furaha kufanya uzinduzi huu kuongeza fursa ya watu kupata mikopo kwa ajili ya elimu” amesema Prof. Mkenda.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo Mhe. Prof. Kitila Mkumbo amesema uzinduzi wa mkopo wa elimu ambao umefanyika leo na NMB kwa kushirikiana na wizara ni jambo jema kwa kuwa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu haijawahi kutosha kwa kuwa mtoaji amekuwa ni Serikali kuu pekee.

Nae Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo ameishukuru Menejimenti ya Benki ya NMB kwa kubaini hitaji kubwa la gharama za elimu kwa wazazi, walezi na vijana nchini na kuona umuhimu wa kushirikiana na Serikali katika kuongeza fursa ya upatikanaji wa fedha kupitia mkopo wenye riba nafuu.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Ruth Zaipuna amesema benki hiyo imetenga Sh Bilioni 200 kwa ajili ya kugharamia elimu na kwamba mkopo huo utatolewa kwa watumishi ambao mishahara yao inapita Benki ya NMB, na inaweza kuchukuliwa kwa kiasi cha kuanzia Sh laki mbili hadi milioni 10 kwa ajili ya mhusika mwenyewe kujiendeleza kielimu ama vijana, Watoto wao hata wenza wao huku akisisitiza kuwa ina riba nafuu ya asilimia 9.