Site icon A24TV News

TANAPA DODOMA WAPEWA PONGEZI KUTANGAZA UTALII WA NDANI KUUNGA JUHUDI ZA RAIS SAMIA SULUHU HA HASSAN

Doreen Aloyce, Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule ameipongeza Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanapa Dodoma kwa jitihada za kuunga juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan kuutangaza utalii wa ndani hapa nchini ambao umepelekea wananchi kuwa na mwitikio kutembelea vivutio mbalimbali.

Kauli hiyo ameitoa jijini Dodoma wakati alipokuwa akiwaaga wadau wa utalii kutoka sehemu mbalimbali wakielekea kutembelea mashamba ya Zabibu kijiji cha Nkulabi kilichopo nje kidogo na mji wa Dodoma ambapo ziara hiyo imeandaliwa na Hifadhi za Tanapa Dodoma kwa kushirikiana na Taasisi ya Dodoma Wine Festival.

Senyamule amesema kuwa uongozi wa Tanapa Dodoma wamekuwa kielelezo kutangaza vivutio vilivyopo ndani ya jiji la Dodoma ambapo wameleta hamasa ya wananchi kuanza kuvitembelea tofauti na hapo awali hawakujua vivutio vilivyopo.

“Niwapongeze sana Tanapa Dodoma mnaunga juhudi za Rais wetu Samia Suluhu Hassan za kuutangaza utalii wa Dodoma na nje tumejionea juzi mlikuwa mnada wa nyama choma Msalato mmewafanya wananchi wajitokeze kwa wingi na leo mmeenda kwenye mashamba ya zabibu ambalo zao hili linapatikana hapa Dodoma na wengi wameonesha kupenda kujifunza namna inavyotengeneza mvinyo,” amesema Rc Senyamule.

Amewataka kuendelea kuhamasisha kutangaza mapori ya wanyama , majengo ya Kiserikali, makumbusho, Jengo la Bunge , jengo la mahakama hivyo vyote ni utalii ambao utawavutia wageni kutoka ndani na nje nchi na itasaidia kuingiza pato la Taifa.

Nae Kamishna mwandamizi Msaidizi wa uhifadhi Tanapa Dodoma Daktari Noelia Myonga amesema kuwa zoezi hilo ni endelevu ambapo wamejipanga kutangaza vivutio vyote vya utalii vilivyopo Mkoa wa Dodoma ikiwa ni njia ya kuwafanya wananchi kuwa na kasumba ya kutalii ,kujifunza kwa faida ya vizazi vijavyo na sio wageni kutoka nje ya nchi kama ilivyozoeleka.

Dkt. Noelia amesema kuwa wananchi watambue kuwa Mkoa wa Dodoma kuna mashamba mengi ya Zabibu, na vivitio vingi ambavyo wanaweza kujipanga kila mwezi kutembelea vivutio hivyo badala ya kusafiri kwenda mikoani.

“Niwasihi wananchi badala ya kukaa mjini kwenye sehemu za starehe na wengine usafiri kwenye Mikoani wakidai hawana pa kwenda ni fursa sasa kutambua kuwa Dodoma kuna vitu vingi vya kutembelea, yakiwemo mashamba ya zazibu ambayo unaweza kutembelea kupata upepo mzuri na kwa utulivu ” amesema Dkt Noelia.

Richie Wandwi Kaimu Mkurugenzi Utalii kutoka Wizara ya mali asili na utalii, Richie Wandwi amesema kuwa katika kupanua wigo wa utalii hapa nchini wamejipanga kukuza utalii wa mikutano na matukio inasaidia kuleta wageni wengi ambapo lengo ni kufikia milioni tano za watalii na fedha za kimarekani bilioni sita ifikapo mwaka 2025.

Mkurugenzi kiwanda cha mvinyo Danfod Semwenda ambaye ni mmiliki wa shamba la Zabibu kijiji cha Nkulabi amesema kuwa Serikali iwasaidie kuboresha zao la zabibu kwa kuwapatia wakulima elimu na dawa ya kuuwa wadudu kwani wengi wao hawana utaalamu wa zao hilo na kupelekea wengi kulima kwa mazoea .

“Kama wakulima watapatiwa elimu itatusaidia kuboresha zao letu na tutapata wageni wengi kuja kutembelea mashamba yetu na tutapata fedha nyingi na kupata masoko ndani na nje ya nchi”amesema

Kwa upande wao watalii Msanii Fredy Ndubaro kutoka Jijini Dar es Salaam na Anna kutoka Dodoma walisema kuwa kupitia utalii wa kutembelea mashamba ya zabibu umeleta tija kwao hasa namna ya kulima zao la Zabibu na utengenezaji wa mvinyo na kuwataka wananchi kupata fursa na familia zao kutembelea mashamba ili wapate elimu.

Mwisho.