Site icon A24TV News

VIJANA WA KIMASAI MORANI WATEMBEZA KICHAPO KWA VIGOGO WA CCM ! WILAYANI MUNDULI ARUSHA

Na Mwandishi wa A24Tv Monduli. Arusha

Viongozi wanane wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Engaruka wilayani Monduli, mkoani Arusha, wamelazwa hospitali baada ya kudaiwa kushambuliwa hadi kujeruhiwa na kundi la wananchi wakati wakifuatilia migogoro ya ardhi.

Habari za kuaminika zinasema kuwa wananchi hao wa Kijiji cha Engaruka Juu, waliwashambulia viongozi hao kutokana na hasira za kuuzwa kwa ardhi ya kijiji hicho kinyemela.

Tukio hilo limetokea juzi jioni wakati viongozi hao ambao ni wajumbe wa kamati ya siasa ya chama hicho walipokwenda kijijini hapo kufuatilia tuhuma za Mwenyekiti wa kijiji hicho, Abrahamu Logolie kudaiwa kuuza ardhi kinyemela.

Hata hivyo, mara baada ya kufika katika kijiji hicho kilichopo takriban kilomita 60 kutoka Monduli Mjini, walivamiwa na kundi la vijana wa kimasai maarufu kama morani zaidi ya 30 waliokuwa wamejikusanya na kuwashambulia.

Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Januari 12, 2022 Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Frank Mwaisumbe amesema miongoni mwa viongozi walioshambuliwa ni pamoja na Mwenyekiti wa CCM wa kata hiyo, Leliya Sengeita pamoja na Katibu wake, Joseph Namoyo ambao walishambuliwa sehemu mbalimbali za miili yao.

Mwaisumbe amesema katika vurugu hizo viongozi hao wamepata majeraha sehemu mbalimbali za miili yao.

“Baadhi wana hali mbaya hivyo wamepelekwa hospitalini kwa matibabu ya haraka,” amesema.

Hata hivyo, Mwaisumbe amedai kuwa uchunguzi wa awali umebaini mwenyekiti wa kijiji hicho, Abrahamu Logolie na viongozi wengine wa Serikali ya Kijiji ndio walioandaa mpango huo wa vijana kuwashambulia viongozi hao wa chama.

Tayari Logolie amekamatwa jana mchana kwa tuhuma za kuchochea mgogoro huo.

“Uchunguzi wa tukio hili umeanza na kuwasaka wote ambao wanatuhumiwa kuhusika na tukio hili japo wengi wamekimbia kujificha porini,” amesema.

Hata hivyo, mmoja wa wakazi wa kijiji hicho Jeremiah Lemosho amedai kuwa tukio hilo limechangiwa na kutoelewana baina ya viongozi wa CCM wa kata hiyo na viongozi wa Serikali ya Kijiji.

“Muda mrefu kuna viongozi wa CCM ndani ya kata wana ugomvi na mwenyekiti wetu nadhani ni mambo ya siasa tu, sasa walipopata malalamiko walipaswa kuwasiliana na viongozi wa serikali ya kijiji ama kata kabla ya kufika huku,” amesema.

Amedai kuwa waliohusika na vurugu huenda ni wafuasi wa Mwenyekiti wa Kijiji na wajumbe wa Serikali ya Kijiji, amekiri uwepo wa migogoro mingi ya ardhi katika kijiji hicho.