Site icon A24TV News

ELIMU YA BIMA KUTOLEWA KWA WANANCHI WOTE

 

Na Geofrey Stephen ,Arusha

Kamishna wa bima nchini ,Dkt Baghayo Saqware amezitaka mamlaka za bima nchini kuendelea kuelimisha wananchi juu ya matumizi ya sahihi ya bima kwa lengo la kuwapunguzia gharama pale wanapofikwa na majanga mbalimbali ikiwemo matibabu ya afya.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wadau wa bima kanda ya Kaskazini,Dkt Saqware alisema pamoja na serikali kuweka mpango mkakati wa ukuzaji na uendelezaji wa sekta ya fedha nchini wa miaka 10 hadi kufikia juni 2030 bado mwitikio wa wananchi ni mdogo.

Alisema mamlaka ya bima nchini inapaswa  kuhakikisha inafikia malengo ikiwemo kuhakikisha asilimia 80 ya watanzania watu wazima wanapata uelewa ifikapo mwaka 2025 pamoja na kuhakikisha asilimia 50 wawe wanatumia huduma ya  bima.

“Lengo lingine ni kuhakikisha bidhaa kumi mpya za bima zinazohitajika  kwa wateja zimeanzishwa ifikapo 2030,kuanzisha mfumo utakaorahisisha kushughulikia madai,malalamiko na utatuzi wake pamoja na kuhakikisha sekta ya hii nchini inachangia angalau asilimia tano ya pato la Taifa kutoka asilimia 1.68,”alisema Dkt.Saqware.

Aliongeza kuwa mikakati hiyo itasaidia katika kuleta tija katika tasnia ya bima nchini na kuweza kufikia hayo ni kuongeza ushirikiano madhubuti wa wadau mbalimbali.

Kwa upande wake Meneja wa mamlaka ya usimamizi wa bima Tanzania(TIRA) Kanda ya kaskazini,Gladness Lema alisema katika kipindi cha mwaka 2021 sekta ya bima imechangia kiasi cha sh.bilioni 50.6 ya mapato ghafi ya bima sawa na asilimia 5.56 ya mapato yote ya sh.bilioni 912.

Aidha alisema kuwa bima za kawaida kanda ya kaskazini ilichangia sh.bilioni 48.9 sawa na asilimia 6.6 ya mapato ghafi yaliyoandikishwa  ya sh.bilioni 746.5 ikiwa mkoa wa Arusha umekuwa wa pili  kwa kuchangia kiasi cha sh.bilioni 42.1 sawa na asilimia 5.64 ya mapato ghafi yote.

“Kwenye bima ya maisha kanda ya kaskazini imechangia sh.bilioni 1.72 sawa na asilimia 1.04 tu ya bilioni 165 zilizoandikishwa  kwenye bima za maisha kwa kipindi hicho na Mkoa wa Arusha umekuwa wanne kwenyw bima ya maisha,”alisema Lema

Alisema takwimu zinaonyesha kwa kipindi cha mwaka 2021 kila mtanzania alitimia wastani wa sh.15334.10 lakini kwa kanda ga kaskazini imeonyesha Mtanzania alitumia sh.10,149.17 katika kununua bidhaa ya bima  kiwango ambapo kipo chini ya wastani wa kiwango cha kitaifa.

Hata hivyo Meneja wa TIRA kanda ya kaskazini alisema mapendekezo yao ni kila kampuni ya bima angalau iwe na mawakala wapya wasiopungua watano ili kufikia idadi ya mawakala 244 ifikapo Desemba 2023 kutoka 134 wa sasa.

“Kila mtoa huduma za bima kuhakikisha anaingiza wateja wapya wasiopungua 20 katika soko la bima,kuongeza bidii katika kutambua fursa za bima zilizopo katika shughuli za kiuchumi kuanzia ngazi za mitaa ,hii ni pamoja na miradi inayotekelezwa ,viwanda,Taasisi,masoko vilivyopo pamoja na shughuli za kibiashara zilizopo katika kukuza uelewa kwenyw eneo hili,”alisema.