Site icon A24TV News

WAKULIMA 200 BUMBULI WANUFAIKA NA ZAO LA CHAI WAMPONGEZA RAIS KWA KUFUFUA KIWANDA

Na John Mhala,Bumbuli

Zaidi ya Wakulima 200 wa Mashamba ya Chai katika kata 14 kati ya kata 18 za  Halmashauri ya Bumbuli Wilayani Lushoto Mkoani Tanga wameanza kunufaika kuuza zao la Chai katika Kiwanda cha Chai cha Mponde kilichofufuliwa na serikali  kwa Uwekezaji wa Shilingi Bilioni 4

Hayo yalisemwa  na Mkuu wa Wilaya ya Lushoto,Kalisti  Lazaro wakati alipotembelea kiwanda hicho kujionea uzalishaji  na kuwataka wakulima kuongeza jitihada zaidi katika kilimo cha zao hilo kwa kuwa wataweza kuuza zao hilo eneo la karibu na kunufaika na kujiinua Kiuchumi.

Lazaro alisema kuwa kiwanda hicho kilisimama uzalishaji miaka 10 iliyopita lakini mwezi mmoja uliopita kimeanza uzalishaji na kuleta faraja kwa wakulima wa Chai ambao walikata tamaa na wengine kuyatekeleza mashamba yao huku wengine wakibalidisha mazao ya kilimo.

Mkuu huyo alisema kuwa hadi sasa ukarabati wa kiwanda hicho umegharimu kiasi cha shilingi miliomi 700 na fedha iliyobaki Shilingi Bilioni 3 zipo kwa ajili ya uwekezaji ,ununuzi wa magari na ujenzi wa nyumba za wafanyakazi.

Akiongelea changamoto ya umeme katika kiwanda hicho alisema kuwa serikali kupitia shirika la umeme Tanzania (TANESCO) lipo katika hatua za mwisho za kuongeza transifoma nyingine ili kuondoa changamoto hiyo ili Kiwanda hicho kiwe na Umeme wa uhakika masaa yote.

Awali Meneja wa kiwanda hicho,Sane Kwilabya alisema kuwa tangu kuanza kwa uzalishaji septembe 2 mwaka huu hadi sasa wamezalisha tani 27,000 za chai na tayari wamepata masoko nchini  Pakstan baada ya kupeleka sampuni za chai ambazo zimekubalika.

Aliwataka wakulima kuchangamkia fursa hiyo kwa kuongeza jitihada za kilimo cha zao la chai ili kuongeza uzalishaji kwani serikali imeamua kuwazawadiwa wakazi wa Lushoto kiwanda hicho kwa lengo la kuongeza thamani ya zao la chai hapa Nchini.

Alisema kwa sasa bado hawajaanza kuajiri rasimu ila wanampango wa kuajiri wafanyakazi watakaofikia 100 na hivyo kupunguza changamoto ya ajira eneo hilo,

‘Niwaambie wakulima waongeze nguvu ya kilimo cha zao la chai kwa kuwa kiwanda kipo kwa ajili yao na uhakika wa soko ,hivyo wachume majani bora yatakayoweza kukinusuru kiwanda kwa kuuza chai iliyobora katika masoko ya kimataifa.

Akiongea kwa niaba ya wananchi  diwani wa kata ya Mponde,Richard Mbughuni alisema kuwa uwepo wa kiwanda hicho kutaimarisha kilimo cha zao la chai na  hivyo  kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na kukuza uchumi wa Taifa.

 

Naye Mwenyekiti wa kijiji cha Mahange,Muhidini Mdoe aliishukuru serikali kupitia mbunge wao Januari Makamba kwamba ameweza kuwasemea vizuri wananchi wake na serikali kusikia kilio chao na kufufua kiwanda hicho.

Alisema yeye kama mwenyekiti atahamasisha wananchi kufufua mashamba ya zao la chai ili wanufaike na soko ambalo lipo karibu.

Ends……