Site icon A24TV News

BILIONEA MPYA APATIKANA! MIRERANI,SERIKALI YANUNUA MADINI YAKE YOTE .

Na Geofrey Stephen Mirerani
Serikali imemtangaza bilionea mwingine mpya wa madini ya Tanzanite, Anselem Kawishe aliyepata mawe mawili yenye uzito wa kilogram 5.22 na thamani ya sh,bilioni 2.25 ambayo yamenunuliwa na serikali.
Katibu mkuu wizara ya Madini, Adolf Nduguru alimtangaza bilionea huyo katika mji mdogo wa Mererani katika hafla ya kumtambulisha bilionea huyo mpya na kununua madini hayo na kusema  kuwa atasaidia kuitangaza Tanzania kimataifa na kufanya sekta ya madini hayo kufahamika zaidi duniani.
Ndunguru alifafanua  kuwa Kawishe alipata vipande viwili vya madini ya Tanzanite vyenye uzito wa kilogramu 3.74 na kilogramu 1.48.
“Kati ya madini hayo mawili, yenye uzito wa kilogramu 1.48 ina thamani ya Sh713.8 milioni na ya uzito wa kilogramu 3.74 yenye thamani ya Sh1.5 bilioni jumla ni Sh2.245 bilioni,” alisema Nduguru.
Alisema Wizara hiyo katika Mwaka wa 2022/23 imejipanga kukusanya mapato ya Zaidi ya Shilingi Bilioni 82
Ndunguru alisema Wizara itafikia malengo hayo kwa kuwa imejipanga katika kuhakikisha inafikia malengo hayo na ikiwezekana kuvunja lengo la makusanyo na hilo linawezekana.
Naye waziri wa Madini Dotto Biteko alisema uuzwaji wa Madini ya Tanzanite vipande viwili Kwa serikali,Waziri Biteko alisema uamuzi wa kuuza Madini hayo umefanywa na Kawishe mwenye kwa kuwa na Imani na Serikali yake na sio vinginevyo
Alisema na kuwataka wachimbaji Wadogo Wadogo wa Madini ya Tanzanite Mirerani kuchimba Kwa juhudi Sana ili Nchi iweze kuibua Mabilionea wengi kwa maslahi ya Nchi.
Waziri ameendelea kuwasisitiza Wachimbaji Wadogo Wadogo wa Madini ya Tanzanite na Wamiliki wa Migodi hiyo kufanya kazi na Biashara Kwa uaminifu Kwa manufaa ya Nchi
” Tuache kufanya Biashara ya Tanzanite Kwa kukiuka Sheria na Kanuni kwani hatutafika na ili tufanye vema Biashara hiyo lazima tufanye Kwa kufuata Sheria na Kanuni” alisema Biteko
Akizungumza Changamoto za Wachimbaji Wadogo Wadogo wa Tanzanite Mirerani alisema karibu zote zimepatiwa ufumbuzi kwani Rais Samia Suluhu Hassan anawapenda.
Katika hatua nyingine waziri Biteko  alisema kuwa serikali iko katika mpango madhubuti wa kujenga Kituo cha Tanzanite City kitakachojengwa katika Mji wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara lengo ni kutaka Madini hayo kuwanufaisha Wafanyabiashara na wachimbaji Wadogo Wadogo wa Madini ya Tanzanite.
Alisema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameshatoa pesa Kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Tanzanite City na Wizara yake ya Madini iko katika hatua ya mwisho mwisho kuhakikisha ujenzi wake unaanza mapema iwezekanavyo.
Biteko alisema lengo la kujengwa Kwa Tanzanite City ni kutaka Madini hayo kuuzwa katika mjii wa Mirerani na Kwa kiasi kikubwa kunufaisha serikali na Wananchi wanaoishi katika Wilaya hiyo na Mkoa Kwa ujumla.
Alisema toka Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani makusanya ya Kodi ya Serikali Kwa Madini ya Tanzanite yameongezeka kutoka Shilingi Bilioni 475 hadi Shilingi Bilioni 625 Kwa Mwaka na hayo ni matanikio makubwa katika sekta ya Madini ya Tanzanite.
Waziri Biteko alisema sekta ya Madini imepanda katika ukusanyaji kutoka asilimia tano hadi kufika asilimia Saba na kufanya uuzwaji wa Madini nje ya Nchi kuwa Mzuri na Wenye tija Kwa serikali.
Naye Bilionea Kawishe akizungumza bàada ya kusaini mkataba wa mauziano na Serikali uliosaini na Gavana wa Benki Kuu, Profesa Florens Luoga Kwa niaba ya Wizara ya Fedha alisema amechimba Madini Kwa Zaidi ya miaka 15 bila mafanikio.
Kawishe alisema baada kufanikiwa kupata kiasi hicho cha Madini amemshukuru Mungu na kusema kuwa atashirikiana na Serikali katika kuhakikisha kila anachostahili kulipa kinalipwa Kwa maslahi ya Nchi.
Mwaka 2020 serikali ilimtangaza bilionea Saniniu Laizer aliyepata mawe yenye ukubwa wa zaidi ya kilogramu 7.8 na kufuatiwa pia na bilionea wa madini ya Ruby Sendeu Laizer akitokea wilaya ya Longido mkoani Arusha.
Mwisho .