Site icon A24TV News

AGIZO LA WAZIRI MKUU UMEME KUFUNGWA SOKO NAMBA 68 KILOMBERO JIJINI ARUSHA SASA MASAA 24

Halmashauri ya jiji la Arusha imeanza kutekeleza kwa kishindo agizo la waziri mkuu Kasimu Majaliwa,la kuweka umeme katika soko namba 68 la Wamachinga, Kilombero Sanjari na kuongeza idadi ya malango ya kuingilia ndani ya soko hilo.
Waziri mkuu Majaliwa alitoa maelekezo mwezi Julai mwaka huu alipofanya ziara ya kutembelea soko hilo ambapo aliagiza uongozi wa halmashauri ya jiji la Arusha kuweka umeme pamoja na kuongeza idadi ya malango ya kuingilia katika soko hilo kama njia mojawapo ya kuliboresha na kurahisisha shughuli za wafanyabiashara hao jambo ambalo limetekelezwa.
Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya jiji la Arusha,Hargeney Chitukulo  amefanya ziara ya kutembelea soko hilo na kueleza kwamba tayari umeme umeingia ndani ya soko hilo upande wa vyoo na kazi inayoendelea kwa sasa ni kuusambaza katika vibanda mbalimbali jambo lililoibua shangwe kwa wamachinga wakimshukuru Mkurugenzi huyo.
Chitukulo alisisitiza kuwa kazi ya kusambaza umeme huo inataraji kukamilika wiki ijayo na utaratibu wa kulipia umeme huo utawekwa na uongozi wa soko hilo.
“Tayari tumeshaanza kutekeleza agizo la waziri mkuu umeme umeshaingia sokoni upande wa vyoo na kazi iliyobaki ni kuusambaza katika vibanda vyote kazi ambayo mpaka wiki ijayo itakamilika”alisema Chitukulo
Hatahivyo,Chitukulo aliagiza uongozi wa soko hilo kuongeza lango lingine la kuingilia ndani ya soko hilo upande wa Mashariki ili kurahisisha shughuli za wafanyabiashara ndani ya soko hilo baada ya kilio cha muda mrefu cha wafanyabiashara  kuhusu uhaba wa wateja unaotokana na uchache wa malango ya kuingilia.
Naye msimamizi wa soko hilo,Sharifa Ayelo alisema kwamba uamuzi wa serikali  kuweka umeme ndani  ya soko hilo utapunguza kero kwa wafanyabiashara  kuchangia sh,500 kwa siku na sasa wataweza kuchangia sh,100 pekee.
“Tumeupokea uamuzi wa serikali kwa mikono miwili kwa kuwa hapo awali wafanyabiashara walichangia sh,500 umeme wa jenereta lakini kwa sasa wanaweza kuchangia sh,100 tu”alisema msimamizi huyo 
Mwenyekiti wa wamachinga jijini Arusha,Amina Njoka aliwataka wafanyabiashara hao kuheshimu sheria na taratibu za kufanya biashara ikiwa ni pamoja na kupanga bidhaa zao kwenye meza na sio kuzipanga chini.
Njoka,alisisitiza kuwa wamejipanga kuhakikisha kero zote  zinatatuliwa ndani ya soko hilo lakini aliwataka wafanyabiashara hao kutopanga biashara zao nje ya soko hilo kama serikali ilivyoagiza na atakayekaidi hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.
Ends…..