Site icon A24TV News

TANZANIA YAENDELEA KUFANYA VIZURI KWENYE MAUZO YA SOKO LA ALMASI DUNIANI.

Na Geofrey Stephen Arusha .

Waziri wa madini nchini,Dotto Biteko amesema kwamba licha ya changamoto ya janga la UVIKO-19 Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika mauzo ya madini aina ya almasi katika soko la dunia.

Waziri Biteko ametoa kauli hiyo leo wakati akifungua mkutano wa tatu wa dharula wa baraza la mawaziri wa jumuiya ya nchi za Afrika zinazozalisha almasi(ADPA) unaofanyika jijini Arusha.

Akizungumza katika mkutano huo waziri Biteko alisema kwamba baada ya janga la UVIKO-19 bei ya almasi duniani ilianguka na kupanda dhahabu lakini kwa sasa almasi imepanda juu na kuifanya Tanzania kuendelea kufanya vizuri duniani.

Waziri Biteko amesema kuwa hivi karibuni kupitia mgodi wa almasi wa Mwadui uliopo mkoani Shinyanga serikal imeuza jiwe moja la almasi lenye kareti sita kwa thamani ya dola milioni 12 katika soko la dunia jambo ambalo linaashiria mafanikio makubwa kwa nchi.

“Huu uzalishaji haujawahi kutokea katika mgodi wetu wa Mwadui kwani tumeuza jiwe moja la almasi ya pink kwa thamani ya dola milioni kumi na mbili haya ni mafanikio makubwa sana kwa nchi yetu “alisema Biteko

Waziri Biteko alisema kwamba pamoja na mgodi wa Mwadui kusimamisha uzalishaji kwa muda kutokana na ukarabati lakini kwa sasa serikali imeongeza hisa kutoka asilimia 25 mpaka 35 kama juhudi za kuongeza uzalishaji wa almasi duniani.

Akizungumzia mkutano wa baraza la mawaziri kwa nchi zinazozalisha almasi barani Afrika waziri Biteko alisema kwamba lengo la mkutano huo ni kuidhinisha nyaraka muhimu za baraza hilo,kuteua sekretarieti sanjari na kuhakikisha nchi za Afrika zinakuwa na sauti moja katika kusimamia rasiliamali hiyo.

Waziri Biteko alisisitiza kuwa wajumbe wa baraza hilo wataupitia upya mfumo wa umoja huo na kujifunza katika eneo la usimamizi wa madini ya almasi barani Afrika.

Alisema kuwa duniani kote madini ya almasi yana urasimu na mlolongo mpana hivyo mkutano huo itawapa fursa wajumbe kusimama na kuangalia vigezo kwa baadhi ya nchi barani Afrika zilizopigwa marufuku kufanya biashara ya almasi duniani.

“Tutaupitia upya mfumo wa umoja wetu ikiwemo katiba na kuboresha miongozo mbalimbali katika eneo la usimamizi wa madini ya almasi Bara Afrika “alisisitiza Biteko

Tanzania ni mwenyekiti na mwenyeji wa mkutano wa ADPA ambapo umoja huo unajumuisha nchi 18 barani Afrika ambapo nchi 12 wanachama na 6 ni waangalizi.

Mwisho