Site icon A24TV News

PANYA TISA WAANZA MAFUNZO KUPAMBANA NA WALIOPATA MAJANGA NA MAGONJWA

Na Joseph Ngilisho, ARUSHA

Wanasayansi na watafiti wa panya kutoka nchi zaidi ya 50 duniani, wamekutana  Jijini Arusha, kujadili namna ya kuwatumia Panya katika udhibiti,kugundua mabomu na kugundua maambukizi ya ugonjwa wa tauni na uokozi wa majanga ya kidunia.

Katika mkutano huo wa saba wa kimataifa wa baiolojia ya panya na udhibiti wa panya duniani, Tanzania imeishangaza dunia, baada ya kufanikiwa kugundua na kuwafundisha panya tisa wa uokozi, kutambua majeruhi na watu waliopoteza maisha katika ajali, hasa kwenye majengo.

Mwenyekiti wa mkutano huo, ambaye ni Mtaalamu wa Utafiti wa Ikolojia ya Panya kutoka Kituo cha Umahiri cha Utafiti wa Panya cha Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Prof. Rhodes Makundi, alisema

“Watafiti hawa wanaangalia mambo tofauti tofauti, kwanza wanaangalia kitu kinachoitwa taxonomy (utambuzi panya wako wa aina gani), pili biodiversity (katika mazingira wanayoishi, kwamba kuna wanyama gani na wanahusianaje),na kingine ni juu ya magonjwa yanayotukabili kutokana na panya.

“Pia, tunaangalia udhibiti wa panya, kwa kutumia njia za kiikolojia, tunaangalia tabia za panya, tunaangalia panya wanaopatikana katika Milima na Mabonde katika Afrika, hasa katika nchi za Afrika ya Mashariki.

Zaidi aliongeza: “Na kingine ni kuangalia matumizi ya panya ili kuleta faida kwa jamii; kwa mfano matumizi ya panya kwenye kugundua mabomu, kugundua ugonjwa wa tauni na mambo mengine, ambayo panya anaweza akatumika.”

Aidha, Prof. Makundi, alisema baada ya mkutano huo wanatarajia, jopo la Wanasayansi hao ambao wamefanya utafiti kwenye nchi tofauti, hasa kudhibiti panya, Wanasayansi wa Tanzania, watajifunza mambo yanayofanyika mahali pengine, na pale inapowezekana utaalamu huo watauchukua kuutumia hapa nchini kutatua matatizo ya panya.

“Kwa mfano, utafiti wa matumizi ya panya kwenye kugundua kutegua mabomu, kugundua magonjwa ya tauni. Unaweza kuona utafiti huo unatumika nchi nyingi kama Cambodia huko.

“Kimsingi, huu ni mkutano ambao una manufaa kwa kila anayeshiriki na jinsi anavyoweza kuutumia katika nchi yake, lakini kubwa kabisa ni ugunduzi mwingi wa kisayansi.”

Akifungua mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela, alisisitiza kuwa kwa sasa umefika wakati, wanasayansi na watafiti hao, kutoka hadharani kuelezea zaidi faida ya eneo hilo ili lisibaki tu kuwa eneo la utafiti.

“Watoke sasa kueleza faida zake ili jamii ielewe zaidi juu ya faida za hili, kwa sababu tunaona kuna hasara nyingi kwenye upoteaji wa mazao na vyakula. 

“Kimsingi wataalamu wetu, Wanasayansi wetu kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, SUA, ndio ambao wanaendesha kwa kiwango kikubwa mkutano huu. Wanasayansi wengu duniani, ambao wako kwenye eneo hili la kutizama athari na faida za panya, ndio dhumuni kubwa.

“Nimeona wanatizama athari wanazoweza kusababisha panya pamoja na faida, kwa sababu ni viumbe ambao ni muhimu kwa maendeleo, na watatizama maeneo yote kimaendeleo, kijamii na kisayansi.

“Mnajua SUA, ndio kitovu cha umahiri kwenye eneo hili la utafiti wa panya, ambao wanatumika kwa matumizi mbalimbali. Sasa hivi matumizi maarufu zaidi ni kwenye kutambua mabomu yaliyotegwa ardhini, lakini vilevile kutambua maambukizi na hali mbalimbali za kifua kikuu.

“Wamekuja wanasayansi wabobezi wakubwa wanashiriki hapa, kwa hiyo hili mimi naliona kubwa sana kwa nchi yetu, kwanza kutambulika kwamba tuna kituo cha umahiri lakini, wanasayansi hawa wote wa dunia, kuja kwetu kutambua nafasi ya wanayasansi wetu wa Tanzania na kubadilishana ujuzi na machapisho mbalimbali na kazi za kisayansi za dunia nzima ambazo zinafanyika kwenye eneo hili, hasa utafiti wa panya.”

 

Akiwa katika mkutano huo, Mtafiti kutoka Shirika la Uhisani la APOPO linalojishughulisha na maisha ya panya, lililopo chini ya SUA, Venance Kiria, alisema shirika hilo limewafundisha panya tisa wa uokozi, ambao mpaka sasa wako kwenye hatua ya mwisho katika ufundishaji.

“Hivi sasa panya hao wa Tanzania, wana uwezo wa kutafuta mtu akiwa umbali mrefu, lakini si kwa kiwango kile ambacho tunakitaka, na hasa kwenye majengo yaliyopata ajali.

“Nimekuja kuwasilisha mada kuhusiana na mkutano wa kimataifa unaoendelea ukihusu kufundisha panya kutafuta watu katika majengo, au ile miundombinu ambayo imeaharibika, baada ya natural disaster mbalimbali (majanga ya asili), kwa mfano tetemeko la ardhi linapotokea.

“Kwa jinsi hali ilivyo sasa kuna ajali nyingi zinatokea sasa hivi kama majengo makubwa ya ghorofa kubomoka. Kwa hiyo mojawapo ya manufaa mbalimbali zinazotokea baada ya hayo majengo kubomoka ni watu kupoteza maisha na wengine kujeruhiwa, lakini wanashindwa kutoka wakisubiri juhudi zetu ili tuweze kuwaokoa wao.”

Mwisho .