Site icon A24TV News

KAMATI YA BUNGE YAIPONGEZA AUWSA! YAITAKA KUSAMBAZA MAJI KWA KASI

Na Joseph Ngilisho, ARUSHA

Kamati ya bunge ya bajeti imeitaka mamlaka ya maji safi na usafi wa Mazingira (Auwsa), katika jiji la Arusha, kuongeza kasi ya usambazaji wa maji safi na salama katika kata ya Muriet  yenye wakazi zaidi ya elfu 60 huku wanaopata huduma hiyo wakiwa ni 400,000 tu.

Mwenyekiti wa kamati hiyo,Daniel Sillo ametoa kauli hiyo wakati alipoongoza ujumbe wa kamati hiyo kwenye ziara ya kutembelea baadhi ya miradi inayotekelezwa na Auwsa jijini Arusha.

Akizungumza mara baada ya kutembelea kituo cha kuuza huduma ya maji kilichopo Muriet Sillo alisema kuwa kutokana na changamoto ya idadi ya wakazi kuwa wengi kuhamia jijini Arusha mamlaka hiyo ina jukumu la kuhakikisha wanasambaza maji safi na salama kwa kasi.

“Kila siku watu wanahamia katika maeneo haya idadi ya watu  inaongezeka hivyo ni  jukumu la Auwsa kuhakikisha wakazi wanapata maji safi na salama”alisema Sillo

Hatahivyo, naibu waziri wa maji nchini,MaryPrisca Mahundi alisema kwamba wizara ya maji imepanga kuhakikisha inaongeza fedha kwenye miradi yote ya maji inayotekelezwa hapa nchini kama ili kuhakikisha haikwami na inakamilika kwa wakati.

“Sisi kama wizara ya maji tumejipanga kuwa sio wizara ya ukame wala malalamiko tutahakikisha miradi yote inayotekelezwa ya maji hapa nchini inaongezewa fedha na inakamilika kwa wakati”alisema Mahundi

Kwa upande wake Mkurugenzi wa mamlaka ya maji safi na taka mkoani Arusha(Auwsa),Justine Rujomba alisema kwamba mamlaka yake iliomba kiasi cha fedha 1.3 bilioni lakini wamepokea 521 milioni kusambaza huduma ya maji katika baadhi ya maeneo jijini Arusha na kwa sasa mradi huo umekamilika kwa asilimia 100.

“Tumetumia sh,700 milioni kusambaza huduma ya maji katika kata ya Terat na maeneo ya jirani na mradi huu umekamilika kwa asilimia 100″alisema Rujomba.

Mbunge wa jimbo la Arusha Mjini,Mrisho Gambo aliiambia kamati ya bunge ya bajeti kwamba serikali inapaswa kuomgeza fedha za kutosha ili kukamilisha miradi mbalimbali ya maji kwa wakati ili kuondoa kusuasua na kutokamilika kwa wakati.

Gambo,alisema kwamba kumekuwa na changamoto ya wakazi wengi kuhamia katika kata ya Terat na hivyo kupelekea huduma ya usambazaji wa maji katika eneo hilo kuwa na changamoto na kuiomba Auwsa kuitazama changamoto hiyo kwa umakini.

Diwani wa kata ya Muriet,Francis Mbise alisema ameridhishwa na kasi ya usambazaji wa maji katika kata ya Muriet na kuiomba serikali iongeze fedha za kutosha ili huduma ya maji iweze kupatikana kwa urahisi kwa kuwa kata yake inaongoza kuwa na idadi kubwa ya wakazi wanaoongezeka kwa kuhamia.

Mwisho