Site icon A24TV News

KAMATI YA YA BUNGE YA BAJETI YAMPONGEZA RAIS KWA FEDHA ZA USTAWI WA TAIFA

Na Geofrey Stephen .Arusha

Kamati ya Bunge ya Bajeti imeipongeza Rais Samia Hassan Suluhu kwa kuhakikisha fedha za Utekelezaji wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19 zinakamilisha ujenzi wa madarasa,maabara na ofisi katika Chuo cha Ufundi Arusha(ATC).

Pongezi hizo zimetolewa Jijini Arusha na Mwenyekiti wa kamati hiyo,Daniel Sillo wakati wa ukaguzi wa jengo hilo lililogharimu sh,bilioni 2.27 ambalo limefikia asilimia 90 ya utekelezaji wake.

Alisema fedha hizo zimesaidia ujenzi wa madarasa nane yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 880 kwa wakati mmoja,maabara sita zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 270 kwa wakati mmoja ikiwemo ofisi 26 zenye uwezo wa kuchukua watumishi 104.

“Hapa tumeona jinsi fedha za Uviko-19 zinavyofanya kazi,tunampongeza Rais Samia kwa kuhakikisha vyuo vya ufundi vinajengwa ili kusaidia jamii kuongeza ujuzi na kuleta tija hapo badae ”

Naye Naibu Waziri wa Elimu,Omary Kipanga aliishukuru serikali kwa kuboresha vyuo mbalimbali ikiwemo kujenga vyuo vinne vya ufundi katika maeneo ambayo hayakuwa na vyuo hivyo ambapo sh,bilioni 20 zimepelekwa kwaajili ya kujenga vyuo vinne katika mikoa ya Rukwa,Geita,Njombe na Simiu.

Aliishukuru Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia kwa kutoa sh ,milioni 523 kwaajili ya kununua samani za majengo katika jengo hilo na kuongeza kuwa mtaala mpya wa elimu utawezesha pia kuwasaidia wanafunzi kupewa ujuzi wa vitu mbalimbali vyenye bunifu zenye tija kwaajili ya kuleta tija kwa wananchi na kuongeza ajira.

Naye Mkuu wa chuo cha ATC, Musa Chacha alishukuru serikali kwa kuhakikisha inaongeza tija kwa vyuo vya ufundi huku akisisitiza kuwa kukamilika Kwa jengo hilo kutapunguza msongamano wa wanafunzi katika madarasa na maabara

Aliongeza kuwa msongamano wa wanataaluma katika ofisi chache pia utapungua sanjari na msongamano wa ratiba za masomo kutokana na uchache wa madarasa na maabara ikiwemo kuondoa baadhi ya vipindi kufundishwa muda wa jioni sana na hata nyakati za usiku.

Nao baadi ya wabunge akiwemo Halima Mdee walikipongeza chuo hicho kwa kuongeza idadi kubwa ya wasichana ambapo katika mwaka wa masomo 2021/22 chuo kinajumla ya wanafunzi 4,693 ikilinganishwa na wanafunzi 2,017 waliokuwepo mwaka 2015/16 ikiwa ni ongezeko la asilimia 132.

Na kuongeza kuwa kunaongezeko la wanafunzi wa kike 769 kutoka waliokuwepo mwaka wa masomo 2015/16 ambao ni 389 sawa na ongezeko la asilimia 97.

Mwisho.