Site icon A24TV News

NAIBU WAZIRI DKT,MOLLEL AZINDUA ZAHANATI ILIYOCHANGIWA NA RAIS SAMIA.

 

Moses Mashalla,Arumeru

Serikali inatarajia kupelekea jumla ya kiasi cha sh,50 milioni kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za madaktari katika zahanati ya Kikatiti ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan aliichangia sh,10 milioni mwishoni mwa mwaka Jana.

Zahanati hiyo kwa Sasa ujenzi wake unafadhiliwa na shirika la misaada la Kikorea la CTSI ambapo limetoa zaidi ya kiasi cha sh,100 kugharamia ujenzi wake huku wananchi wakichangia kiasi cha sh,63 milioni ambapo pia shirika hilo lilisaini makubaliano ya ushirikiano(MOU) baina yake na halmashauri ya Meru.

Akizindua zahanati hiyo hivi karibuni naibu waziri ya afya nchini,Dkt Godwin Mollel aliiagiza bohari kuu ya dawa za serikali kuhakikisha wanaleta vifaa haraka pindi ujenzi utakapokamilika.

Mbali na kutoa ahadi hiyo Dkt Mollel alisema kuwa serikali inatazamia kuibadilisha zahanati hiyo kuwa kituo cha afya ili iweze kutoa huduma kwa wananchi wengi zaidi.

Akizungumza Mara baada ya kuzindua zahanati hiyo Dkt Mollel alisema kwamba zahanati hiyo ni muhimu kwa wakazi wa eneo la Kikatiti na hivyo serikali itafanya kila namna ianze kufanya kazi kwa haraka.

Alisema kuwa zaidii ya kiasi cha sh,1.5 bilioni zimetolewa na serikali kwa lengo la kuboresha sekta ya afya wilayani Arumeru na hivyo serikali imajidhatiti kuhakikisha suala la afya kwa wakazi wa Arumeru ni kipaumbele.

“Nawaagiza Msd kwamba zahanati hii ikishakamilika mlete vifaa hapa haraka tunataka hii zahanati ianze kuhudumia wananchi kwa haraka” alisema Dkt Mollel

Naye Rais wa shirika la misaada la Kikorea ,Kyung Chul Kam alisema kuwa shirika lao litaendelea kushirikiana na halmashauri ya wilaya ya Meru katika kusaidia miradi mbalimbali.

“Tutaendelea kushirikiana na Tanzania ikiwemo halmashauri ya Meru katika kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo kama uchimbaji wa visima,elimu,afya” alisema Kam

Mkuu wa wilaya ya Arumeru ,Mhandisi Richard Ruyango alisema kuwa serikali wilayani Arumeru itahakikisha inasimamia mazingira bora kwa wawekezaji wote wilayani humo ili waweze kufanya kazi zao bila usumbufu kama agizo la Rais Samia.

Mhandishi Ruyango alimpongeza mkurugenzi wa halmashauri ya Meru ,Mwalimu Zainab Makwinya huku akisisitiza kuwa fedha zote zilizotolewa na serikali kwa ajili ya kuboresha sekta ya afya zitasimamiwa kikamilifu.

Hatahivyo,diwani wa kata ya Kikatiti,Kisari Nyiti alisema kuwa fedha iliyotolewa na Rais Samia sh,10 milioni mwaka Jana ndio imekuwa kichocheo cha ujenzi wa zahanati hiyo mpaka Sasa.

Alisema kuwa wananchi wa kata yake wamechangia jumla ya kiasi cha sh,63 milioni huku akimwomba naibu Waziri Dkt Mollel kuwasaidia kukamilisha kipande cha chumba cha akinamama kujifungulia ombi lililopokelewa na Dkt Mollel.

Mwisho.